Afisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Swissport Tanzania Bw. Gaudence Temu
(Katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya
utendaji wa kampuni yake mara baada ya mkutano mkuu wa kampuni hiyo
kumalizika uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Pamoja nae
kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Swissport, Bw. Juan Jose Andres Alvez na
Bw, Jeroen L. de Clercq ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo
nchini Kenya.
KAMPUNI ya
Swissport Tanzania Plc imepata ongezeko la faida kwa asilimia 73 (baada
ya makato ya kodi na gharama nyingine zote), mafanikio yaliyotokana na
maendeleo makubwa ya Sekta ya Usafiri wa Anga hapa nchini.
Kampuni
hiyo inayotoa huduma zake kwenye viwanja vya ndege vya Julius Nyerere
(JNIA), Kilimanjaro pamoja na ule wa Mtwara, ilitangaza mafanikio hayo
hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake mkuu wa
thelathini.
Akizungumza
mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo,
Bw Juan Alvez alitaja sababu za mafanikio hayo kuwa ni pamoja
na kuongezeka kwa mashirika ya ndege yanayofanya safari zake katika
viwanja vya ndege vya Tanzania na ongezeko la wingi wa safari kwa
mashirika yaliyopo.
“Ongezeko
hili la asilimia 73 ni matokeo ya ongezeko la faida kutoka sh. bilioni
7.496 mwaka 2013 hadi kufikia sh. Bilioni 12.937 iliyoripotiwa mwaka
2014,’’ alisema.
Akifafanua
zaidi Bw Alves alisema jumla ya abiria 1,111,156 walihudumiwa katika
kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambao ni sawa na ongezeko la asilimia
23 ikilinganishwa na idadi ya abiria 905,347 waliohudumiwa katika
kipindi cha mwaka 2013.
Kufuatia
mafanikio hayo ambayo pia yameonekana kwenye idara nyingine ikwemo ya
ubebaji wa mizigo, Bw Alves alisema wana hisa wa kampuni hiyo wana kila
sababu ya kutabasamu kwa kuwa watapokea Sh287.50 ya gawio kwa kila hisa
ikilinganishwa na sh 166.58 ya mwaka 2013 ili kuhakisi ongezeko hilo la
asilimia 73.
Akizungumzia
uwekezaji uliofanywa na kampuni hiyo kwa 2014, Afisa Mtendaji Mkuu wa
kampuni hiyo Bw. Gaudence Temu alisema kampuni hiyo ilifanikiwa kununua
vifaa vya usaidizi ardhini (GSE) vyenye thamani ya sh. Bilioni 1.7huku
akiongeza kuwa vifaa hivyo tayari vimeshafika na vimeanza kutumika.
“Ongezeko
lingine la sh. bilioni 2.7 katika uwekezaji linatarajiwa kufanyika
ndani ya mwaka huu na litahusisha mabasi mawili ya kubebea abiria katika
viwanja vyetu sambamba na kifaa cha kupakia na kushusha mizigo mizito
chenye uwezo wa hali ya juu,’’ alibainisha Bw. Temu.
Kampuni
hiyo inajumuisha pia wanahisa wa Kitanzania wapatao 11,500 ambao
wanamiliki asilimia 49 ya hisa zote huku asilimia 51 zikiwa zinamilikiwa
na kampuni ya Swissport International.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...