1
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa amri kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam leo April 28, 2015
2
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mara baada ya kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam leo April 28, 2015
34
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata picha ya kumbukumbu na makamanda wa meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam leo April 28, 2015
5
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Chifu Edward Wanzagi wa kabila la Wazanaki (kati) pamoja na Mbunge wa Afrika Mashariki Mhe Makongoro Nyerere baada ya kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam leo April 28, 2015. PICHA NA IKULU
---------------------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,  Jumanne, Aprili 28, 2015, ametoa kamisheni na kuruhusu kuanza kutumika kwa Melitiva mbili kwa ajili ya ulinzi wa pwani ya Tanzania.

Rais Kikwete ametoa kamisheni hiyo na kuruhusu kuanza kutumika kwa meli hizo, Melivita P77 Tanzania Navy Ship Mwitongo na Melivita P78 Tanzania Navy Ship Msoga katika Sherehe ya Utoaji Kamisheni iliyofanyika Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Maji la Tanzania Navy Base, Kigamboni, mjini Dar es Salaam.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Davis Mwamunyange na Balozi wa China katika Tanzania, Balozi Lu Youching walikuwa miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo pamoja na wawakilishi wa kijiji cha Mwitongo, Butiama Mkoani Mara na Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani ambavyo majina yake yametolewa kwa meli hizo mbili.

Akizungumza katika sherehe hizo, Jenerali Mwamunyange amesema uongozi wa Jeshi umeamua kuziita meli hizo mbili kubwa zaidi za kivita zilizopata kununuliwa nchini majina ya vijiji walikozaliwa viongozi wakuu wawili wa Tanzania, Mwalimu Nyerere na Rais Kikwete.

Rais Kikwete ameambiwa katika shehere hizo kuwa meli hizo kutoka Jamhuri ya Watu wa China, zitaongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa JWTZ kulinda mpaka wake ulioko katika Bahari ya Hindi na kuweza kukabiliana zaidi na vitendo vya uharifu, ugaidi na  kulinda vizuri zaidi shughuli za utafutaji gesi na mafuta katika pwani hiyo ya Tanzania.

Akizungumza kabla ya kutoa kamisheni kwa meli hizo, Rais Kikwete ameishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika Nyanja ya kijeshi na Nyanja nyingine nyingi.

“Marafiki zetu wa China wamekuwa nasi kwa muda mrefu, wametuunga mkono tokea kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tokea Mwaka 1964. Kwa upande wa ulinzi wa majini, wamekuwepo tokea Mwaka 1971 walipotusaidia kuanzishwa kituo hiki cha Tanzania Naval Base hapa Kigamboni na kutoa boti 13 za ulinzi.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Wamesaidia vifaa, wamesaidia utaalam na wataalam, wametoa mafunzo katika Chuo chetu cha Ubaharia cha hapa hapa. Kwa hakika hakuna marafiki kama wenzetu wa China, wananchi wake na Serikali yake kwa sababu wamesaidia sana maendeleo ya Jeshi letu. Karibuni wametusaidia kuanzisha kombania mbili za majeshi maalum ya majini na sasa meli hizi mbili ambazo zina uwezo wa kwenda kasi zaidi, uwezo wa kubeba silaha nyingi na kubwa zaidi na uwezo zaidi wa kulinda mipaka yetu”.

“Wako watu wanasema kuwa vifaa vya jeshi na ulinzi wa nchi yetu ni ghali. Ni kweli. Lakini sasa nani atatulindia nchi yetu? Ni sisi wenyewe na kazi ya ulinzi wa nchi haiweza kuwa kazi rahisi, wala nyepesi, wala isiyokuwa na gharama.”

Akifafanua hali ilivyo katika Pwani ya Tanzania, Rais Kikwete amesema: ”Miaka ya karibuni hapa yaliwahi kutokea majaribio 28 ya kuteka nyara meli katika eneo la maji la Tanzania, matano yalifanikiwa na mengine yakashindikana. Tuna shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, maharamia  hufanya jitihada za kuzivuruga, lazima tuzilinde.”

Akitoa kamisheni hiyo, Rais Kikwete amesema:  “Kwa kutumia nafasi yangu kama Amiri Jeshi Mkuu, natoa kamisheni na kuruhusu kuanza kutumika kwa melivita P77 Mwitongo na P78 Msoga. Mwenyezi Mungu azibariki melivita hizi pamoja na wafanyakazi wake wote.”

Wakati wa ukaguzi wa meli hizo, Rais Kikwete ameambiwa kuwa kila moja ya meli hizo ina uwezo wa kukaa baharini kwa muda wa siku saba bila kuhitaji kuongeza mafuta wala diseli na bila kuhitaji msaada wa huduma yoyote kwa ajili ya watumishi wake.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

28 Aprili,2015


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Maafa ya majini yakitokeaga..huwa tu wapweke kama hatuna navy.........

    ReplyDelete
  2. avenue na ndege .za kisasa kila la kheri .TZ

    IPO siku tutazpga mkwara nchi jiran kama kenya heshma silaha tu

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...