HATIMAYE hatma ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba na mjumbe wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Dk Damas Ndumbaro itatolewa Mei 10 mwaka huu.
Kikao cha Kamati ya rufaa ya nidhamu chini ya Revocatus Kuuli ilisikiliza hoja za pande mbili ambao Ndumbaro alijiwakilisha mwenyewe wakati kwa upande wa TFF iliwakilishwa na wakili wao Emmanuel Muga huku habari za ndani zikidai kuwa licha ya Ndumbaro kukata rufaa, TFF nayo imemfungulia shtaka la tatu la kuandaa mechi kinyume na taratibu.
Kikao hicho kilipitisha taratibu za kisheria ambazo zitatumika kuamua kesi hizo ambazo ni taratibu kama zinazotumika mahakamani ikiwemo kuwasilisha hoja zao kwa mdomo na si maandishi kitendo ambacho kimekubaliwa na pande zote mbili.
Wakili wa TFF, Emmanuel Muga aliiambia Mwananchi kuwa taratibu hizo zimewekwa ili kuondoa malalamiko kwa pande zote mbili.
"Ni taratibu tu kama za mahakama za kawaida, hii inasaidia kuepusha manung'uniko upande mmoja kulalamika kuonewa."alisema Muga.
Awali rufaa hiyo ya Ndumbaro ilikuwa ijadiliwe Aprili 12 lakini Sekretarieti ya TFF ilizembea kupeleka barua ya wito wa kuitwa kwenye rufaa hiyo kitendo ambacho Ndumbaro alikigomea kwa kile alichoeleza kuwa hawezi kuburuzwa.
"Mimi ni mwanasheria, kanuni na taratibu nazifahamu, nilikata rufaa TFF walitakiwa waniletee samas wiki moja kabla angalau ili nijue na nijipange sasa mtu anakukurupusha kwa simu unatakiwa kwenye kikao leo hii mimi ni mtu mzima siwezi kuburuzwa."alisema Ndumbaro.
Kitendo hicho cha Ndumbaro kugomea kudhuria kikao, kiliilazimisha kamati hiyo ya rufaa kutoa agizo kwa TFF kumpa tarifa ya wito Ndumbaro kabla ya Aprili 14 na juzi Jumapili Ndumbaro aliudhuria kikao hicho na sasa hatma yake itajulikana Mei 10.
Ndumbaro alikata rufaa ya kufungiwa miaka saba na Kamati ya Nidhamu baada ya kutiwa hatia kwa makosa mawili.
Hatua hiyo imekuja baada ya Ndumbaro kugomea agizo la TFF juu ya kukatwa asilimia 5 za mgao wa fedha za klabu kutoka kwa wadhamini wa ligi kuu ambapo baadaye shirikisho hilo lilimburuza kwa Kamati ya Nidhamu kwa kitendo chake cha kukiuka kanuni zao.
TFF ilimshitaki Ndumbaro kwa makosa mawili ambayo moja ni kutoa taarifa zisizo sahihi kiasi cha kupotosha kuhusu uamuzi wa TFF juu ya kanuni mpya za ligi kuu 2014/15 kinyume na kifungu namba 41 kifungu kidogo cha sita huku shitaka la pili likiwa kutamka kuwa kanuni za ligi hiyo siyo halali huku akijua kuwa zimepitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF ambayo yeye ni mwanafamilia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...