Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), imealika wataalamu wa kilimo ili kuchambua na kutoa mapendekezo juu ya namna bora nchi inavyoweza kutatua changamoto ya masoko kwa wakulima. Ili kufikia lengo hilo, maabara ndogo ya siku tano imeandaliwa ili kutathmini mifumo ya sasa ya masoko kwa mazao ya mahindi na mpunga.  

Akifungua maabara hiyo jijini Dar es Salaam, Jumatatu, Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Omari Issa amewataka wadau wote husika kufanya kazi hiyo kwa pamoja katika kuleta majibu yanayolenga mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuwapatia nafuu wakulima.
  
Alisisitiza kuwa nidhamu ya kiutendaji ya BRN inawataka wadau wa sekta za umma na binafsi kufanyakazi kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazozikabili sekta muhimu; ikiwemo ya kilimo na kuongeza kuwa majibu ya changamoto za masoko kwa wakulima yatakoka kwenye pande pande hizo mbili. Maabara hiyo ndogo inajumuisha wawakilishi 50 kutoka sekta za umma, binafsi, taasisi za kimataifa na wakulima wenyewe. 

Tanzania nzima, na hususani miradi ya kipaumbele ya kilimo iliyo chini ya BRN, ilishuhudia uzalishaji mkubwa wa mahindi na mpunga katika msimu wa 2013/14; jambo ambalo limeleta fursa nzuri lakini pia lilikuja na changamoto zake. Kwa mfano katika msimu huo, uzalishaji wa mahindi ulifikia tani milioni 6 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani milioni 4.5 kwa wastani katika miaka mitano ya nyuma. Mpunga ulifikia tani milioni 1.7 kutoka tani milioni 0.85 mwaka uliotangulia. 

Mwisho wa maabara hii, washiriki wataibua mapendekezo na mpango wa utekelezaji utakaoainisha mfumo madhubuti wa masoko ya mahindi na mpunga. Inatarajiwa kwamba mapendekezo haya yataweza kutumika kwa mazao mengine pia. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...