.jpg)
Sababu za kuanzisha mfumo huu
mpya zinalenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi katika kufikisha huduma kwa
wateja, kuongeza ufanisi katika mchakato wa ajira, Kupunguza muda wa mchakato
wa Ajira ili kukidhi mahitaji ya wadau, kuwafikia waombaji wa nafasi za kazi
wengi zaidi, kudhibiti udanganyifu wa sifa toka kwa waombaji wa fursa za Ajira
kwa kurahisisha ukaguzi na uhakiki wa taarifa za waombaji kazi kwa kuunganishwa na mifumo ya taasisi
mbalimbali lakini pia kukidhi maelekezo ya Sera mbalimbali za utumishi wa umma pamoja
na dira ya Taifa ya mwaka 2025 kuhusiana na umuhimu wa matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano katika kutimiza malengo ya Taifa.
Hadi sasa Sekretarieti ya
ajira imefanya majaribio ya kupokea maombi ya kazi kwa kutumia mfumo wa “Recruitment
Portal” kwa matangazo ya kazi matano ambayo yaliyowahusu waajiri mbalimbali
serikalini na muitikio umeonekana kuwa mzuri.
Matangazo hayo yalihusu Wakala
wa serikali mtandao lililotolewa tarehe 22 Aprili, 2014 ambapo kati ya nafasi 12
zilizotangazwa idadi ya maombi yaliyopokelewa yalikuwa 1,158, Tangazo la nafasi
za Mkemia mkuu wa Serikali lililotolewa tarehe 4 Desemba, 2014 lenye nafasi 11
jumla ya maombi ya kazi 119 yalipokelewa kwa njia ya mtandao.
Matangazo mengine ni ya Mamlaka ya Hali ya hewa la tarehe 4 Desemba,
2014 lililokuwa na nafasi moja na idadi
ya maombi ya kazi matatu yaliyopokelewa, tangazo la tarehe 16 Januari, 2015 la
Wizara ya Ardhi lililokuwa na nafasi 51 ambalo jumla ya maombi ya kazi 738
yaliwasilishwa na tangazo la mwisho lilitolewa tarehe 10 Machi, 2015 kwa niaba
ya taasisi mbalimbali Serikalini jumla ya maombi ya kazi 2,567 yalipokelewa
kutumia mfumo huu. Idadi hii inaonyesha kuwa watu wengi wameanza kuhamasika na
matumizi ya mfumo huu.
Taratibu za uzinduzi rasmi wa
mfumo huu inatarajiwa kufanyika hivi karibuni ambapo sekretarieti ya ajira
inatarajia kupunguza muda wa uendeshaji wa
mchakato wa ajira kwa asilimia 34%. Aidha mfumo pia utapunguza
changamoto kadhaa zikiwemo baadhi ya barua kutofika kwa wakati au kupotea kwa
kutumia njia ya posta, Mrundikano wa barua na nyaraka nyingine zinazohusiana na
maombi ya kazi kutokana na matumizi ya
karatasi, Barua za vibali vya ajira kuwasilishwa wakati vimechelewa na
kusababisha mchakato kuchelewa na gharama inayotokana na uendeshaji wa mchakato
mzima wa ajira kuwa juu.
Pia mfumo huu utakuwa rafiki
na rahisi kwa watumiaji kwa kuwa wataweza kutumia simu zao za kiganjani kupata
taarifa za mchakato wa ajira kila wakati kwa kupiga *152*00#
Tunatoa rai na kusisitiza
kuwa waombaji kazi na wale wanaotarajia kuingia katika soko la ajira wajisajili
katika mfumo huu kwa kufungua http://portal.ajira.go.tz ili
kuingiza taarifa zao za kitaaluma,
wasifu binafsi (CV) pamoja na vyeti.
Matarajio ya Sekretarieti ya
ajira ni kuona kuwa mara baada ya mfumo huu kuzinduliwa rasmi utaongeza ufanisi,
ubora, uwazi na uwajibikaji wa huduma zinazotolewa, kupunguza muda unaotumika
sasa wa kuendesha mchakato wa ajira, Gharama za uendeshaji zitapungua kwa kiasi
kikubwa na mfumo utawafikia waombaji wa fursa za kazi wengi zaidi na kwa
haraka.
Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma inapenda kuwasisitiza wananchi hususani
waombaji kazi kuwa inaendelea na uimarishaji wa mfumo mpya wa kutuma maombi ya
kazi kwa njia ya mtandao (recruitmemnt portal) ili kuondoa baadhi ya changamoto
zilizojitokeza baada ya majaribio kabla ya uzinduzi wake na tunasisitiza na
kuhimiza waombaji kazi pamoja na wanafunzi wanaotarajia kumaliza vyuo waendelee
kujisajili katika mfumo huo mpya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...