Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dr. Margaret F. Chan amemteua Dr. Winnie  Mpanju-Shumbusho kutoka Tanzania kuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani, upande wa masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika. Uteuzi huu umetangazwa rasmi na Dr. Chan wakati wa kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Shirika la Afya Duniani kilichoanza tarehe 14 mpaka tarehe 26 Mei 2015, Geneva, Uswisi.

Dr. Mpanju-Shumbusho ni mtaalamu na kiongozi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika ngazi za juu za uongozi katika sekta ya Afya na Ushirikiano wa Kimataifa.

Kabla ya uteuzi huu, Dr. Mpanju-Shumbusho alikuwa Naibu wa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi ndani ya Shirika la Afya Duniani upande wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika na akiwa na cheo cha Ukurugenzi wa Idara inayoshughulikia Ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani na Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund to Fight AIDS, Tuberculosis na Malaria). Dr. Mpanju-Shumbusho pia ni mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani kwenye Bodi ya Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na Bodi mbalimbali za kimataifa.

Hapo awali, Dr. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya kudhibiti Ukimwi na magonjwa mengine husika katika ya Shirika la Afya Duniani (WHO), makao makuu Geneva, Uswisi.

Kabla ya kujiunga na Shirika la Afya Duniani, amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa East, Central and Southern Africa Health Community Secretariat yenye makao makuu yake, Arusha, Tanzania. Vilevile, aliwahi kuwa Mkuu wa Idara na Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Afya ya Jamii na Mgonjwa ya Watoto, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Muhimbili University of Health Science). Katika wadhifa huu, Dr. Winnie pia alikuwa mwanzilishi wa mipango mbalimbali ya Afya na taaluma na Mshauri Mkuu wa Wizara ya Afya, Tanzania upande wa Afya ya Jamii. Pia amewahi kuwa mjumbe wa Bodi mbalimbali za kimataifa.

Dr. Mpanju-Shumbusho ana Shahada ya Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; vilevile ana Shahada ya Uzamili katika Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Tulane, Marekani na Shahada ya Uzamili katika Medicine (Paediatric and Child Health) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vilevile ana Shahada ya Uzamifu na Shahada nyingine mbalimbali.

Akiwa Mkurugenzi na mtaalamu katika Shirika la Afya Duniani, amekuwa mstari wa mbele katika kuandaa, kuongoza na kutekeleza mipango mkakati ya Dunia ya kujenga na kuimarisha sekta ya Afya hususani katika nchi maskini na zile zinazoendelea. Mipango hii imezaa mafanikio makubwa ikiwemo kujenga uwezo wa nchi maskini kukabiliana na maradhi ikiwemo pia afya za kina mama na watoto. 

Sambamba na hilo, mipango hii pia ilifanikisha upatikanaji wa madawa ya gharama nafuu katika nchi maskini ili kuweza kumudu gharama za matibabu kwa watu maskini. Nchini kwetu, Dr. Mpanju-Shumbusho ameweza kufanikisha upatikanaji wa matibabu na huduma nasaha za kusaidia kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na magonjwa yaliyosahaulika.

Dr. Shumbusho ameolewa na ana watoto wawili, wa kiume na kike.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 22, 2015

    Hongera saba Dr. Winnie Mpanju. Mungu akutangulie.MDAU SCANDINAVIA.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 22, 2015

    Hongera sana Dr. Winnie Mpanju Shumbusho. kila la kheri kazi majukumu yako mapya. Tunahitaji wantanzania wengi kwenye Taasisi za Kimataifa kama ulivyowewe. Hivyo wakati ukitekeleza majukumu yako, ombi letu kama Tanzania na watanzania, fungua milango kwa Watanzania wengine ili nao waweze kujiunga na Taasisi kama hizo hiyo ndiyo itakuwa moja ya Legacy yako.

    Tunakuombea kwa Mungu na tunakutakia kila la kheri.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 22, 2015

    Legacy yake iwe determined Na utendaji wake bora wa kazi kuahikikisha kuwa afya za wote na hasa nchi maskini zinaimarika. Utendaji wake bora na sio utaifa pekee ndio uliomfikisha hapo alipo. Na kama watanzania kama tutafanya kazi kwa bidii na ufanisi ktk nafasi zetu kwa kufuata nayo zake sioni kwa nini tusipate nafasi ktk mashirika ha kimataifa tuwe watanzania ama la?

    ReplyDelete
  4. Mama yangu! sikujua akina mama wako zaidi waliofikia viwango kama hivi. Kama wengine pia wangetokezea tukajua viwango kama hivi mbona kina mama tunahaki ya kujidai!! You are a role model Dr. Mpanju. Mwenyezi Mungu azidi kukutangulia katika majukumu haya.

    Mary Kalikawe

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 22, 2015

    Mpendwa Dr. Winnie Mpanju-Shunbusho, Hongera sana. Bwana akutangulie kama wakati wote na kukujalia hekima katika utekelezaji wa majukumu yako mapya. Wote hapa nyumbani (Ma Nyin'Abarongo na Nyin'Abarongo) na wote tunakuombea afya njema na mafanikio. Keep the fire burning Doctor!!!!

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 23, 2015

    Hongera sana Dr. Mpanju, Mungu azidi kukuinua katika maisha yako. Tunakukumbuka wakati upo tz unatutibia tukiwa wadogo. Hongera sana ila pia wewe ni kichwa si mchezo.

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 23, 2015

    Tunakuombea HERI mama yetu,,Mungu awe nawe katika kila ufanyalo kwaajili ya umma

    ReplyDelete
  8. AnonymousMay 27, 2015

    Wow HOngera sana Dr. Winnie, namfahamu dr toka Arusha back then. Kweli fanya kazi kwa bidii na kwa moyo wote Mungu atakupa tuzo kupitia watu wake.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...