KISOMO cha kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha aliyekuwa mwimbaji mahiri nchini, marehemu Amina Ngaluma ‘Japanese’ kinatarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii Kitunda, Machimbo Dar es Salaam.
 
Akizungumza baba mzazi wa marehemu,  Kassim Ngaluma, alisema kisomo hicho kitafanyika nyumbani kwa wazazi wake marehemu na kuwaomba ndugu, jamaa na marafiki mbalimbali wa marehemu wakati wa uhai wake wahudhurie.
 
“Tunaomba wote tulioshiriki kwa namna mbalimbali wakati wa msiba wa marehemu mwanangu, tushirikiane pia katika kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo chake,” alisema Mzee Ngaluma na kuongeza kuwa kisomo hicho kitafanyika saa saba mchana baada ya swala ya adhuhuri.
 
Aliwaomba waliokuwa wanamuziki wenzake na marehemu, mashabiki wake, pamoja na wadau wengine wa muziki na marafiki wote, washirikiane katika tukio hilo.
 
Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Mei 15 mwaka jana kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor na kuzikwa Mei 24 mwaka huo, Dar es Salaam.
 
Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’, Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya.
 
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize.
 
Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili,  Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...