Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Mhe. Bernard K. Membe jana aliongoza
Jopo la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki nchini Burundi kwa lengo la kupata hali ya maendeleo ya kisiasa
nchini humo.
Wakiwa nchini humo,
mawaziri hao walikutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais
wa Jamhuri ya Burundi, viongozi na wawakilishi wa vyama arobaini na tano vya
siasa vya upinzani nchini humo, ambapo walitoa salamu za Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Waziri
Membe, kwenye mazungumzo yao na Rais Nkurunziza yaliyodumu takriban saa moja na
nusu, mawaziri hao walifikisha mwaliko kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,
kuhudhuria Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi ambao umepangwa kufanyika Dar es
Salaam Mei 13, 2015.
Kwenye jopo hilo la
mawaziri liliongozwa na Mhe. Bernard Membe wa Tanzania, walikuwepo pia Mhe.
Balozi Amina Mohamed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya na Mhe. Louise Mushikiwabo,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda
aliwakilishwa na Rtd Brig. Matayo Kyaligonza Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini
Burundi.
“Lengo kuu la mkutano
huo utakaofanyika jijini Dar es salaam ni kujadili hali ya amani wakati wa
kuelekea kipindi cha uchaguzi nchini Burundi” Waziri Membe aliwaeleza waandishi
wa habari waliokuwa wakimsikiliza baada ya mazungumzo hayo.
Kwenye mazungumzo
hayo ya Burundi Waziri Membe alimuomba Rais Nkurunziza na viongozi wa vyama vya
siasa nchini humo kutoa maelezo, na maoni yao kwa jopo hilo kwa uwazi na
kupendekeza namna ambavyo viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakavyoweza
kuisadia Burundi.
Pande zote mbili
zilizoshiriki kwenye mazungumzo hayo na jopo la mawaziri kwa nyakati tofauti
walielezea kufurahishwa kwao na hatua ya Rais Kikwete kuitisha kikao hicho cha
Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili suala la
Burundi kwa wakati muafaka.
Hadi wakati
mazungumzo hayo, wakimbizi wapatao ishirini na nane elfu wameikimbia nchi hiyo
kwenda Rwanda na Tanzania ambapo wengi wao wameingia nchini Rwanda.
“Hili ni janga la
kibinadamu ambalo ni lazima jumuiya yetu chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya
Kikwete kulipatia ufumbuzi kwa haraka” alimalizia Waziri Membe.
Kwenye safari hiyo,
Waziri Membe aliongozana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama (NUU) pamoja
na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mhe. Leticia Mageni Nyerere (Mb.).
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO YA
SERIKALI KWA UMMA,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
07 MEI 2015
Afrika ya mashariki iwe ni ukanda wa Afrika wa amani.
ReplyDelete