Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu  ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi hiyo Bw. Morrice Oyuke.
Wadau mbalimbali na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015.

Na. Veronica Kazimoto.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Sheria Mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 haina lengo la kuzuia Taasisi au watu binafsi kufanya tafiti zao hapa nchini bali inalenga kuweka misingi imara ya shughuli za kitakwimu na tafiti zenye ulinganifu unaotokana na mfumo rasmi utakaoondoa uwepo wa takwimu zinazokinzana. 
 Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria hiyo mpya iliyoridhiwa na Bunge Mwezi Machi mwaka huu
Amesema kuanzishwa kwa sheria hiyo kunalenga kutoa mwongozo kwa Taasisi za Serikali na Mashirika mbalimbali yanayozalisha takwimu hapa nchini ili yaweze kuendesha shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa takwimu kwa kuzingatia sheria hiyo mpya na kuwa huru kutoa takwimu sahihi  zinazoendana na uhalisia wa Tanzania. 
“Sheria hii hailengi kuondoa uhuru wa taasisi nyingine za utafiti za utafiti zilizopo kisheria kufanya kazi zao, taasisi hizo zitaendelea kuwa huru kufuata taratibu zao ilimradi hazikiuki sheria hii” Amesisitiza Dkt.Chuwa.
Amefafanua kuwa kifungu cha 20 cha sheria hiyo,kinaeleza kuwa takwimu zinazotolewa na taasisi zilizo nje ya Serikali lazima zikidhi vigezo vya kitakwimu vilivyowekwa na NBS ili ziweze kutumika kupanga mipango ya maendeleo.
 Kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofanya tafiti mbalimbali chini ya wahadhiri wa vyuo vikuu Dkt. Chuwa amesema ipo sheria inayowalinda na kusimamia matokeo ya tafiti zao zinazosambazwa kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha vyuo vikuu.
Ameongeza kuwa sheria hiyo katika kifungu cha 37 (3) imeainisha makosa mbalimbali na adhabu ya kifungo kisichopungua miezi 6 au faini isiyopungua shilingi milioni moja.
Ameyataja makosa hayo kuwa ni upotoshaji wa ukweli kuhusu takwimu rasmi utakaofanywa na vyombo vya habari, vitendo vya kuzuia msimamizi, mdadisi au karani wa Sensa kutekeleza majukumu yake kisheria,kukataa kwa makusudi kujaza fomu au nyaraka yoyote au kujibu maswali yaliyoulizwa, kutoa taarifa zisizo sahihi, kuharibu fomu au nyaraka yoyote na  mtu yeyote kujifanya msimamizi , mdadisi au karani wa Sensa kwa lengo la kupata taarifa ambazo hastahili kuzipata.
Makosa mengine ni yale ya kushawishi mtu asishiriki katika zoezi la kitaifa Kitakwimu litakaloendeshwa na Ofisi hiyo kwa mujibu wa sheria hiyo, kukataa kutoa nyaraka zozote zinazohitajika katika shughuli za kitakwimu na kukiuka kifungu chochote cha sheria hiyo.
Kuhusu mchakato wa kupatikana kwa sheria hiyo amesema umezingatia vigezo vyote ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kupitisha muswaada wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 katika Mkutano wake wa 19 na kisha kujadiliwa  Bungeni, Muswaada huo kuwasilishwa kwa wadau ambao waliujadili na kutoa maoni ambayo yalisaidia kuboresha muswaada huo.
Amesema kuwa kutakuwa na kamati maalumu ya kitaalam itakayoundwa kwa ajili ya kuangalia takwimu zitakazokuwa zinakusanywa ili kuhakikisha kuwa hakuna ukiritimba wowote unaojitokeza katika kuthibitisha na kupitisha tafiti na takwimu zitakazowasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Amesisitiza kuwa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo kuzumgumza na vyombo vya habari ili kujenga uelewa wa umuhimu wa sheria hiyo kwa maendeleo ya Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 20, 2015

    Kwa kweli tatizo kubwa kwetu sisi watanzania ni style yetu ya kuchagua wabunge kwa sifa nyinginezo pasipo kuzingatia iwapo ni intellectuals. Sasa kwa upeo walio nao wao wameona hii sheria ni sawa ipitishwe sasa ni too late, tujilaumu wenyewe, mlaumu mbunge wako uliyemchagua na ameipitisha. Jirani zetu welevu na intellectuals wa Kenya na Uganda sheria kama hizi hazina nafasi wala kufikiriwa. JoeSheffu (Dar)

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...