Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Ali Hassan Mwinyi amefanya ziara ya siku tatu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ziara hiyo ya Rais Mstaafu inafuatia mwaliko wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliomuomba kuwa mgeni mashuhuri katika sherehe za kuadhimisha miaka hamsini na mbili (52) ya Afrika.

 Siku ya Afrika huadhimishwa tarehe 25 Mei na mataifa ya Afrika pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa mataifa hayo duniani kote, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kuasisiwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) tarehe 25 Mei 1963.

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina desturi ya kuungana na Waafrika pamoja na wadau wengine wanaounga mkono hatua za ukombozi na kupinga ubeberu katika maadhimisho ya siku hii muhimu.

Katika sherehe hizo, Rais Mstaafu Mwinyi alihutubia hadhira iliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Dkt Muhammad Javad Zariff na kuhudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi waliopo Iran, Viongozi na Maafisa waandamizi wa Serikali ya Iran, na wadau wengine muhimu ikiwemo wanataaluma, wawakilishi wa sekta binafsi na wanahabari.

Aidha, Rais Mstaafu Mwinyi alipata nafasi ya kukutana na Mkuu wa Kamisheni ya Usuluhishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye pia ni Rais Mstaafu wa taifa hilo Ayatollah Hashemi Rafsanjani. 

Ayatollah Rafsanjani alikuwa Rais wa Iran wakati Ali Hassan Mwinyi akiwa Rais wa Tanzania na wawili hao waliimarisha uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa haya mawili ambapo kila mmoja alizuru nchi ya mwenziwe. Rais Mstaafu Mwinyi aliupokea mwaliko wa taifa hilo kwa lengo la kuzidi kuimarisha uhusiano wa kidugu baina ya Tanzania na Iran. Katika ziara hiyo, Rais Mstaafu Mwinyi aliongozana na Mke wake, Mama Khadija Mwinyi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...