Maisha Lab ya Uganda wametangaza kuwa warsha yao nyingine itafanyika Zanzibar wakati wa ZIFF 2015 mwezi Julai kuanzia tarehe 18 hadi 25. Maombi toka kwa wanaotaka kushiriki katika warsha hii yameanza kupokewa na mwisho wa maombi ni tarehe 13 Juni.

Warsha za Maisha Lab zimekuza vipaji vya waandishi wa filamu na wakurugenzi wa filamu wengi hapa Afrika Mashariki. Tayari warsha hizo zimefundisha zaidi ya watu 1000 tangu Maisha Lab ianzishwe. Mkurugenzi wa Maisha Lab aliyeko Kampala Uganda alisema kuwa wanataraji kutoa skolaship 60 kwa wanafunzi kwa mwaka kwa washiriki toka nchi zote za Afrika Mashariki.

“Katika warsha zetu watu 60 (15 toka kila nchi) watachaguliwa kuhudhuria mafunzo hayo yatakayoongozwa na wakufunzi waliobobea katika fani za uandishi wa filamu. Nia ni kuongeza ujuzi na kupanuwa wigo wa biashara ya utengenezaji filamu hapa Afrika Mashariki.” Alisema Fibby Kioria Mkurugenzi wa Maisha lab.

Katika kila Warsha script zitashindanishwa na mshindi atapatiwa $5000 ili kumwezesha kutengeneza filamu fupi katika mwaka unaofuata. Mwaka jana Nassir Qassim wa Tanzania ndiye aliyeibuka mshindi.

Hii ni warsha ya 3 itakayofanyika Zanzibar na ZIFF ndio mdhamini wake ili kuwapa washiriki nafasi ya kushiriki katika tamasha na hivyo kuweza kukutana na watengeneza filamu wengine toka nje wanaokuja kwa ZIFF. Pia wanapata nafasi ya kuangalia filamu tele zinazoonyeshwa wakati wa Tamasha.

Lakini Mkurugenzi wa ZIFF aliharakisha kusema kuwa anasikitishwa sana kuona kuwa washiriki toka Zanzibar huwa wachache kila mwaka. “Tunajuwa kuwa waandishi wa filamu toka zanzibar wanahitaji sana mafunzo haya maana yanawapa ujuzi na pia nafasi ya kujuana na watengeneza filamu wengine wa kimataifa”, alisema Mkurugenzi huyo.

Tasnia ya filamu ya Bongo Movies imesemwa sana kwa kuwa na hadithi dhaifu kimataifa. Kwa kutumia warsha kama hizi wadau wanaweza kukuza vipaji vyao na kufikia hadhi ya kimataifa.

ZIFF mwaka huu imejitolea kuwasaidia wale wote ambao wangependa kutuma maombi yao ili kuwasaidia kufuata malekezo ya usaili, kuwapa miongozo ya uandishi wa skripti na kuwaongezea nafasi za kuchaguliwa kuhudhuria warsha hii muhimu. 

Wanaotaka kusaidiwa katika hili wanatakiwa kufika ZIFF, Ngme Kongwe Zanzibar, au kutuma maombi yao ya kusaidiwa kwa barua pepe workshop@ziff.or.tz

Wanaotaka kujua zaidi kuhusu warsha hii waingie kwenye tovuti hii: www.maishafilmlab.org au wawasiliane na fibby@maishafilmlab.org

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...