Wizara ya Afya Zanzibar imesema Kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kinaendelea
kufanya kazi zake za kutoa Matibabu Masaa 24 kama
kawaida kwa kufuata utaratibu maalum uliowekwa Hospitalini hapo.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
Chukwani wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku
Hashim Ayoub aliyetaka kujua lini Serikali itaweka daktari katika Hospitali
hiyo kwa Masaa 24.
Amesema Hospitali ya Mnazi
Mmoja ni Hospitali Pekee ya Rufaa kwa Zanzibar
ambayo inafanya kazi ya kutoa huduma bora za afya na kwamba kwa sasa ina
Madaktari bingwa wa Mifupa Wawili wanaopatikana kwa muda wa Masaa 24.
Amefahamisha kuwa kwa sasa
Hospitali ya Mnazi Mmoja inautaratibu maalum wa Madaktari wa zamu kwa kila
Idara kuwepo Hospitali kwa masaa 24 ili kuweza kutoa huduma pindipo anapofika
mgonjwa.
Awali Jaku alidai kuwa Wagonjwa
wa Ajali wanaofika kutafuta huduma kwa Madaktari hao wa Mifupa wanasumbuka na
kupata huduma siku ya pili jambo ambalo halipendezi kwa Hospitali hiyo ya
Rufaa.
Hata hivyo Naibu WAziri wa
Afya alisema wagonjwa wote wanaofika Hospitali wakiwemo wagonjwa wa ajali
hutakiwa wapitie kitengo cha huduma za dharura (Emergency department) kwa
kupatiwa matibabu ya haraka zaidi katika kitengo hicho ambacho Madaktari hupatikana
kwa masaa 24 .
Waziri Mahmuud aliongeza kuwa
Hospitali hiyo imeweka usimamizi maalum kwa kufuatilia kazi za kila siku kwa
watendaji wake na kuweza kutatua tatizo lolote linapotokezea.
Kuhusu malalamiko ya Madaktari
Naibu Waziri huyo amewashauri Wananchi kupeleka malalamiko yao katika Ofisi ya Daktari Mkuu katika Jengo
la Utawala Hospitalini hapo ili yaweze kufanyiwa kazi
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...