Rais Jakaya Mrisho Kikwete
ametuma salamu za rambirambi kwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC), Bw. Clement Mshana, wafanyakazi wake na waandishi wote kwa ujumla
kufuatia kifo cha mtangazaji na mwandishi mwandamizi wa TBC Bi. Florence
Dyauli (pichani enzi za uhai wake).
“Pokea rambirambi zangu za dhati
kwa kuondokewa na mwandishi mwandamizi na mahiri Bi. Florence” Rais amesema
“Mbali na uandishi na
utangazaji wake mahiri, Bi. Florence alikua mzalendo wa kweli aliyetumikia
taasisi hii ya serikali kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na
tutaukosa mchango wake. Ni wajibu wetu kumuombea mapumziko mema kwa mwenyezi Mungu
na kumshukuru kwa mchango wake alioutoa kwa moyo wa dhati”. Amesema Rais Kikwete na
kuongeza kuwa:
“Hakika Florence tutamkumbuka,
nawapa pole wafanyakazi wote wa TBC na waandishi wote kwa kuondokewa na mwenzao
katika tasnia ya Habari”.
Rais ameongeza.
“Salaam pia ziwafikie ndugu na
jamaa wa Bi. Florence ambao msiba huu ni mkubwa sana kwao na unawagusa sana,
naelewa machungu waliyonayo na huzuni, hata hivyo kwa pamoja ni wakati wa
kuzidi kumuombea Marehemu katika safari yake ya mwisho”. Rais amesema na kuwatakia
roho ya subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao.
Bi. Florence ambaye amefariki
jana 18 Juni, 2015 jijini Dar-es-Salaam
alizaliwa Julai 27, 1961. Bi. Florence alianza kazi katika Radio ya Taifa,
Radio Tanzania Dar-es-Salaam (RTD) na baadaye
Televisheni ya Taifa (TVT) na kwa sasa TBC .
Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya
Marehemu mahali pema peponi, Amina.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...