Na Greyson Mwase, Bagamoyo
Taasisi zinazohusika na usimamizi wa sheria na kanuni za mazingira zimetakiwa kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mazingira migodini na kuepuka mwingiliano wa majukumu.
Wito huo umetolewa na Kamishna Msaidizi wa Madini – Ukaguzi wa Migodi Mhandisi Ally Samaje katika mahojiano maalum kwenye mafunzo yanayohusisha Makamishna Wasaidizi wa Madini, Wakaazi kutoka Wizara ya Nishati na Madini Tanzania na wataalam kutoka India yanayoendelea mjini Bagamoyo mkoani Pwani.
Mhandisi Samaje alitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii (Misitu) na kuongeza kuwa taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala muhimu yahusuyo madini hususan katika masuala yenye kuhitaji uelewa wa pamoja.
 Wakati huo huo akizungumza kwa kutumia mfano wa nchi ya India, mtaalam mwelekezi kutoka Taasisi ya Sayansi na Mazingira kutoka Nchini India, Sujit Kumar alisema kuwa India ina taasisi nyingi mbalimbali zinazohusika katika usimamizi wa kanuni na sheria za mazingira hali inayopelekea ugumu katika usimamizi wa sheria na kanuni hizo.
“ Matokeo yake kila taasisi inaona kuwa sheria na kanuni zake za mazingira ni bora na sahihi na kuwataka wawekezaji wa madini kuzifuata, hivyo kupelekea ukaguzi wa migodi kuwa mgumu.” Alisisitiza Singh.
 Naye mtaalam muelekezi kutoka Taasisi ya Sayansi na Mazingira ya Nchini India, Srestha Banerjee akizungumzia jinsi ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kutumia mfano wa nchi ya India alisema kuwa ili wachimbaji wadogo waweze kufanikiwa kupata leseni wanatakiwa kuunda vikundi vidogo vidogo na kuomba leseni ya pamoja na kuanza kumiliki vitalu.
Banerjee alishauri serikali kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia ruzuku kwani wana mchango mkubwa sana katika pato la nchi kupitia sekta ya madini.
 Alisisitiza kuwa elimu ni muhimu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa wengi hawana elimu hali inayopelekea kuchimba katika mazingira hatarishi na kutokea kwa ajali za mara kwa mara migodini.
 Ili kuhakikisha kuwa wananchi waishio karibu na migodi wananufaika na rasilimali za madini, Banerjee alipendekeza kuanzishwa kwa mifuko ya madini ambapo fedha zinazolipwa kama kodi na wawekezaji zitawanufaisha wananchi wote.
 Alisema kuanzishwa kwa mifuko itakayowanufaisha wananchi kutachochea maendeleo katika ngazi ya halmashauri na wananchi kuondokana na dhana kuwa hawanufaiki na rasilimali za madini.
 Aliongeza kuwa fedha hizo zinaweza kutumika katika uboreshaji wa huduma za jamii kama vile maji, umeme, miundombinu, afya pamoja na kusomesha wakazi kupitia elimu za madini.1
Mijiolojia wa Wizara ya Nishati na Madini, Assa Mwakilembe akizungumzia sekta ya madini  nchini kabla ya kumkaribisha  Kamishna Msaidizi – Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje  ili aweze kufungua mafunzo kwa wataalam wa Wizara. Mafunzo hayo yaliyoshirikisha Makamishna Wasaidizi kutoka Ofisi za Madini Nchini  na kufanyika Bagamoyo mkoani Pwani, yanatolewa na Taasisi ya  Sayansi na Mazingira kutoka  India, lengo likiwa ni kubadilishana  uzoefu na kuwapa uelewa katika usimamizi wa mazingira kwenye migodi.2
Kamishna Msaidizi – Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje kutoka  Wizara  ya Nishati na Madini akifungua mafunzo yaliyoshirikisha Makamishna Wasaidizi kutoka Ofisi za Madini Nchini yanayoendelea mjini Bagamoyo mkoani Pwani.3
Kamishna Msaidizi – Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje kutoka  Wizara  ya Nishati na Madini (wa kwanza kushoto, waliokaa mbele) pamoja na washiriki wengine wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa na wataalam kutoka  Taasisi ya  Sayansi na Mazingira kutoka Nchini India (hawapo pichani) katika mafunzo kuhusu usimamizi wa mazingira migodini yanayoendelea mjini Bagamoyo mkoani Pwani.4
Sehemu ya wataalam kutoka Idara ya Madini iliyopo chini ya  Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia kwa makini mada kuhusu usimamizi wa mazingira kwenye migodi katika nchi  ya India iliyokuwa inawasilishwa na mtaalam mwelekezi kutoka  Taasisi ya Sayansi na Mazingira ya Nchini India, Sujit Kumar Singh (hayupo pichani) kwenye mafunzo  hayo.5
Mtaalam kutoka  Taasisi ya Sayansi na Mazingira ya Nchini India, Srestha Banerjee akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.6
Mtaalam mwelekezi kutoka  Taasisi ya Sayansi na Mazingira ya Nchini India, Sujit Kumar Singh akisisitiza jambo katika mafunzo hayo.7
Kamishna Msaidizi – Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje kutoka  Wizara  ya Nishati na Madini (wa tatu kutoka kushoto, waliokaa mbele), Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka Wizara  ya Nishati na Madini,Mhandisi  Gideon Kasege ( wa pili kutoka kulia, waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo  hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...