Na. Mwandishi Maalum.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,
Idara ya Uratibu maafa imefanikiwa kupunguza athari za maafa yatokanayo na
ukame wilayani Kishapu kwa kutumia jumla ya Shilingi milioni 207 kwa kutekeleza
Mradi wa Kuijengea Jamii Uwezo wa Kupunguza Athari za Maafa yatokanayo na ukame
wilayani humo kwa kuijengea jamii uwezo
wa kupata uhakika wa chakula na kipato.
Mradi huo umetekelezwa kwa mafanikio katika kata 3 za Mwamalasa,
Masanga na Langana, ambapo
vikundi vya maendeleo kumi (10)
vyenye jumla ya wanachama 100 vimefanikiwa
katika ufugaji wa Mbuzi na kuku, kilimo
cha viazi, mtama, mboga mboga pamoja, upandaji wa miti kwa uhifadhi wa mazingira na utengenezaji mtandao
wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Akiongea wakati wa mafunzo ya waratibu maafa na wataalum katika
ngazi za kata, Shinyanga tarehe 25 Juni, 2015, Mratibu maafa Wilayani Kishapu,
Ponsian Kuhabwa amefafanua kuwa fedha hizo zilizotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
kwa menejimenti ya maafa ya ukame
zimefanikisha kata 3 zinazotekeleza mradi huo kupata uhakika wa chakula na
kipato.
Kuhabwa; “Fedha tulizozipata katika kipindi
cha miezi sita ambacho tumetekeleza mradi huu tumeweza kutoa mafunzo ya menejimenti ya maafa
ya Ukame kwa wataalamu wa ngazi za kata, mafunzo ya Ugani, kununua pembejeo, vifaa na dawa za mifugo, kupitia mradi huu tunao
mbuzi 1050, kuku 1800 ikiwa awali
walipatiwa mbuzi 550 na kuku 550 hali ambayo huzifanya kata hizo kutoathiriwa
na ukame.”
Mkazi wa kijiji cha Masanga, kata ya
Masanga, wilayani Kishapu, Magreth William, amebainisha kuwa ukame uliokuwa
ukiikumba kata hiyo mara kwa mara, walikuwa wanapata athari za upungufu wa
chakula pamoja na kutokuwa na kipato kutokana na mazao yao ya biashara kuharibikia
mashambani.
William; “Tumeweza kupunguza athari za
maafa ya ukame kupitia mradi huu kwa kuwa tunao uhakika wa chakula kwa kuwa
tunalima mazao yanayo himili ukame kama mtama na viazi lishe lakini pia tunao
uhakika wa kipato kwa kuwa tunafuga mbuzi na kuku hivyo pamoja na ukame
unaendelea kujitokeza lakini kwa sasa hatuathiriki kama awali”.
Mradi wa Kuijengea Jamii Uwezo wa
Kupunguza Athari za Maafa kwa Mikoa iliyoathirika zaidi na ukame unafadhiliwa
na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri
Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji wakuu wa mradi huo.
Mradi huo
unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, ulizinduliwa wilayani Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba,
2013.
Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Mradi
wa Kuijengea Jamii Uwezo wa kupunguza Athari za Maafa kwa Mikoa iliyoathirika
zaidi na Ukame, , Harrison Chinyuka
akisisitiza jambo wakati
wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa Wataalam na waratibu maafa mkoani
Shinyanga tarehe 25, Juni, 2015.
Mratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara
ya Uratibu maafa, Theodosia Mbunda akifanya majadiliano na washiriki wa mafunzo
ya menejimenti ya maafa mkoani Shinyanga wakati wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa
na Ofisi hiyo kwa waratibu wa Maafa
mkoani Shinyanga tarehe 25, Juni, 2015.
Mshiriki wa mafunzo ya Menejimenti ya
maafa mkoani Shinyanga, Pastor Mphoy akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo
yaliyoratibiwa na Ofisi hiyo kwa
waratibu wa Maafa mkoani humo tarehe 25, Juni, 2015.
Mkuu wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Jamii,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Hellen Msemo, akifanya majadiliano na
washiriki wa mafunzo ya menejimenti ya maafa mkoani Shinyanga wakati wa mafunzo
hayo yaliyoratibiwa na Ofisi hiyo kwa
waratibu wa Maafa mkoani Shinyanga tarehe 25, Juni, 2015.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...