THE UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425 |
|
PRESIDENT’ SOFFICE,
STATE
HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko
njiani kwenda India ambako atafanya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne
katika Jamhuri ya India kwa mwaliko wa Rais wa India, Mheshimiwa Pranab
Mukherjee. Ziara hiyo, inaanza rasmi jioni ya leo, Jumatano, Juni 17, 2015.
Wakati
wa ziara yake, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, mbali na
kukutana na Rais Mukherjee kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali, atakutana kwa
mazungumzo na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mohammad Hamid Ansari na Waziri Mkuu
Narendra Damordadas Modi, ambaye aliingia madarakani rasmi Mei 26, mwaka jana,
2014 akiwa Waziri wa 15 wa Jamhuri ya India baada ya chama chake cha Bharatiya
Janata Party (BJP) kushinda
uchaguzi mkuu.
Ziara
hii itakuwa ya pili kwa Rais Kikwete kutembelea India katika miaka 10 ya
uongozi wake. Mwaka 2008, Rais Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
(AU), alitembelea India ambako alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kwanza
wa Wakuu wa Nchi za Afrika na India (India-Africa Forum) uliofanyika mjini New
Delhi, mji mkuu wa India pamoja na Waziri Mkuu wa India wakati huo, Mheshimiwa
Manmohan Singh.
Wakati
wa ziara yake, Rais Kikwete atatembelea miji ya New Delhi na Jaypur (Pink City
of India) na miongoni mwa shughuli zake ni kukutana na Watanzania ambao
wanaishi India, kukutana na wafanyabiashara wakubwa wa India wenye kutaka
kuwekeza Tanzania na na kufungua Mkutano wa Kwanza wa Wafanyabiashara wa
Tanzania na India (1st Indian-Tanzania Business Forum).
Mbali
na wafanyabiashara, kiasi cha wanafunzi 2,500 wa Kitanzania wanasoma katika
vyuo vikuu vya India kwa ufadhili wa Serikali za Tanzania na India. Hawa ni
mbali na maelfu ya wanafunzi ambao wanajisomesha wenyewe katika vyuo vikuu vya
nchi hiyo.
Rais
pia atakutana kwa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la India, Air
India, kwa nia ya kulishawishi shirika hilo kuanzisha tena safari za ndege kati
ya nchi hizo mbili, atakutana na Mtendaji Mkuu wa Benki ya ICICI, benki kubwa
binafsi kuliko zote katika India, ambayo inataka kuingia ubia na Benki ya Posta
Tanzania, atakutana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Infrastructure Leasing and
Financial Services ambayo inataka kujenga barabara ya kisasa kabisa
kati ya Dar es Salaam na Chalinze na miradi mikubwa ya maji.
Aidha,
Rais Kikwete atakutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni ya Hospitali
za Apollo ambayo inataka kujenga hospitali kubwa na ya kisasa Kigamboni, Dar Es
Salaam.
Rais
Kikwete pia atatembelea kiwanda cha kutengeneza matrekta cha Fiat
New Holland ambacho kimekuwa kinashirikiana kwa karibu na Kampuni ya
Biashara ya Jeshi la Kujenga Taifa ya SUMA JKT na baadaye kutembelea Shirika la
Taifa la Viwanda Vidogo la India.
Rais
Kikwete ataungana na Waziri Mkuu Modi kushuhudia utiaji saini wa mikataba minne
kati ya Tanzania na India katika maeneo ya utalii, maji na miundombinu.
Ziara
ya Rais Kikwete katika India inatoa nafasi ya kuimarisha uhusiano wa
kihistoria, wa karibu na wa kirafiki ambao una historia ndefu na ya karne
nyingi na ambao uliimarishwa zaidi na
uhusiano rasmi ambao ulianzishwa miaka 54 iliyopita. Kimsingi uhusiano huo
umejengwa katika misingi ya biashara na mahusiano ya watu kwa watu.
India
ndiyo nchi inayofanya biashara kubwa zaidi duniani na Tanzania. Mwaka 2013-14,
biashara hiyo ilikadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni nne. Mbali na
uhusiano wa biashara, Watanzania wengi wamekuwa wanasaka huduma za afya na
elimu katika India. Inakadiriwa kuwa tokea mwaka 1999 kiasi cha Watanzania
4,100 wamepata huduma za afya katika hospitali za Apollo pekee.
Inakadiriwa
kuwa kuna wananchi kati ya 50,000 na 60,000 wenye asili ya India (PIO’s) ambao
wanaishi na kufanya kazi katika Tanzania.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Juni, 2015.
Yafaa sana Rais wetu afuatilie ya Waafrika wenzetu walioko India, yaani, wale waliohamia huko kabla ya Enzi za utumwa, wakati wa utumwa na baada ya utumwa: WASIDI au SIDIS.
ReplyDeleteHatukubali kuwa na uhusiano mzuri na India, endapo wenzetu hayo wanasahauliwa. Hawa ni damu moja na makabila mengi ya pwani ya Afrika Mashariki.