Shirika lisilo la Kiserikali la Oxfam hapo jana lilikabidhi vituo vya kusindika maziwa kwa wanawake wa vikundi vinne kutoka vijiji vya Engaresero, Pinyinyi, Malambo na Piyaya vilivyoko katika wilaya ya Ngorongoro.
Akipokea vituo hivyo kwa niaba ya wanavikundi hao, Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro John Kulwa Mgalula, alisema ana imani vituo hivi vitawasaidia wanawake kukua kiuchumi na kuepuka kuwa tegemezi kwani wanawake wengi wamekuwa na sifa ya uvumilivu, uangalifu wa hali ya juu na kwamba mara nyingi wao hufanya vitu kwa uaminifu.
Mkurugenzi aliyashukuru mashirika ya Oxfam waliofadhili ujenzi wa vituo hivi pamoja na PALISEP waliotekeleza mradi huu kwa jitihada mbalimbali ambazo yamekuwa yakifanya katika wilaya ya Ngorongoro ili kuwakuza wanawake kiuchumi huku akitaja miradi mingine iliyofadhiliwa na Oxfam kuwa ni pamoja na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula, ujenzi wa majosho, pamoja na ujenzi wa vyanzo vya maji.
Akikabidhi vituo hivyo, Stellah Julius kutoka Oxfam alisema, “Baada ya kufanya utafiti uliowashirikisha wanawake wa vijiji hivi vinne walituambia kwamba wanahitaji vituo vya kusindika na kuhifadhia maziwa. Tumewajengea vituo hivi mvitumie kwa maendeleo yenu.” Stellah pia aliipongeza serikali na wadau mbalimbali kwa kutoa ushirikano mkubwa uliopelekea kufanikisha ujenzi wa vituo hivyo ikiwemo kutoa maeneo ya ardhi ya vijiji hivyo vinne.
Aidha Stellah aliwataka wanavikundi hao kuwa wabunifu wa namna ya kujiendeleza kibiashara na kuepuka kutegemea mashirika na taasisi ambazo zipo kwa muda tu.
Naye Mkurugenzi wa shirika la PALISEP Robert Kamakia alisema shirika lake limewajengea uwezo wana vikundi hao kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na mbinu mbalimbali za kibiashara pamoja na kuwafundisha namna za kutunza maziwa kwa usafi.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngorongoro
John Kulwa Mgalula akijalibisha Jokofu linalotumia umeme wa jua wakati wa uzinduzi huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...