Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe 4 June 2015 bila kupingwa wakati
wa Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani
(WMO-Congress wa 17) ulioanza tarehe 25 Mei ambao unatarajiwa kumalizika tarehe
12 Juni, 2015 jijini Geneva, Uswisi.
Kuchaguliwa kwa Dr.
Agnes Kijazi kumetokana na jitihada kubwa za Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wetu
wa Kudumu Umoja wa Mataifa, Geneva.
Dr. Kijazi anaongoza
ujumbe wa Tanzania katika ushiriki Mkutano huo ambao una washiriki kutoka Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Wizara ya Maji na Ubalozi wa Tanzania, Geneva.
WMO ni Shirika la Umoja
wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya hali ya hewa duniani na mabadiliko ya
tabia nchi. WMO inatekeleza majukumu na maamuzi kuhusu maendeleo ya sayansi ya
hali ya hewa na uboreshaji wake ikiwa ni pamoja na kusimamia viwango katika
upimaji na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama.
Hadi wakati wa Mkutano
huu unaoendelea nchini Uswisi, WMO ilikuwa na nchi wanachama 191. Katika
Mkutano huu nchi za Sudani ya Kusini na Tuvalu zilikaribishwa rasmi kama
wanachama wapya wa WMO. Kati ya nchi hizi 191 Wanachama wa WMO ni nchi 37 tu ambazo
zina wajumbe katika Baraza hilo kuu. Hivyo hii ni nafasi adhimu na heshima kwa
Tanzania, TMA na Dr Kijazi ambaye ni msomi mwenye utaalamu wa kutosha akiwa na
shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika sayansi ya Hali ya hewa.
Kazi kuu ya Baraza la
Utendaji la WMO, ambalo Tanzania imefanikiwa kuwa mjumbe ni kuchukua hatua
zinazostahili, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Shirika hilo kutekeleza
maamuzi yanayotolewa na Mkutano Mkuu (WMO-Congress) ambao hukutana mara moja
kila baada ya miaka minne.
Akizungumza baada ya
uchaguzi huo Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa
Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa alielezea sababu ya Tanzania kugombea nafasi hiyo muhimu ni kutaka
kuwa ndani ya chombo cha maamuzi na hivyo kushawishi maamuzi yatakayoinufaisha
jamii nzima ya kimataifa ikiwemo Tanzania katika masuala ya hali ya hewa ikiwa
ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kisayansi katika kukabiliana na athari za
mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea maeneo mengi Duniani. Aidha, Dkt.
Kijazi alieleza kuridhishwa kwake na jinsi ambavyo nchi wanachama 190
walivyoridhishwa na utendaji wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu
(2012-2015) ambacho alikuwa mjumbe wa Baraza hili na hivyo kumchagua tena
katika kipindi kingine cha miaka minne. “Hii ni heshima kubwa kwa nchi yangu ya
Tanzania na ninaahidi kutumia uwezo wangu wote kutekeleza majukumu ya nafasi
hii” alisema Dkt. Kijazi.
Dr. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ndiye aliyechaguliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council) la Shirika la Hali ya Hewa Duniani–World Meteorological Organization (WMO) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2015 hadi 2019.
Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...