Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Watanzania waishio Uholanzi waliojitokeza kumlaki wakati akiwasili jijini The Hague, Uholanzi, leo Jumatatu Juni 8, 2015.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo na muhtasari wa ziara yake toka kwa Balozi wa Tanzania nchini Uholani Mhe Wilson Masilingi baada ya kuwasili The Hague leo Jumatatu Juni 8, 2015.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC Jaji Silvia Alejandra Fernandes de Gurmendi alipotembelea makao makuu ya mahakama hiyo jijini The Hague leo Jumatatu Juni 8, 2015.
Rais Jakaya Kikwete akiongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Mhe. Bert Koenders jijini The Hague leo Jumatatu Juni 8, 2015.
Watanzania wanaoishi nje ya Nchi wangependa serikali ijayo iendeleze na
kudumisha juhudi za kuimarisha uchumi kuanzia pale ambapo Rais Jakaya
Mrisho Kikwete ameishia katika utawala wake.
Jumuiya ya Watanzanzia wanaoishi nchini Uholanzi (TANE)
wamemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika risala yao iliyosomwa na
Makamu Mwenyekiti wa Mpito Bwana Johannes Rwanzo, ambapo Rais amepata
fursa ya kuzungumza na Watanzania hao jioni ya tarehe 8 Juni2015, katika
Hoteli ya Crowne Plaza, mjini The Hague .
"Tunaomba serikali ijayo iendeleze pale utakapoishia". Amesema Bw.
Rwanzo. “Tunajua kuna mambo mengi ambayo labda muda wa awamu mbili
hautoshi kuyakamilisha, basi tungeomba mambo haya uweze kuyakabidhi
kwenye utawala unaofuata ili waendeleze pale utakapokuwa umefikia"
ameongeza.
Bw. Rwanzo ameyataja baadhi ya mambo ambayo yanahitajika
kuendelezwa na awamu ijayo kuwa ni pamoja na juhudi za kupambana na
umaskini nchini na ujenzi wa miundombinu.
Watanzania hao pia wamemuomba Rais Kikwete kuwa, pamoja na
kustaafu, bado wangependa aendelee kutoa msaada kwa wananchi wa
Tanzania kwani "Kustaafu sio mwisho wa kusaidia jamii".
Tangu kuingia madarakani, Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa
kukutana na Watanzania wanaoishi nje ya Nchi kila anapofanya ziara katika Nchi
mbalimbali na kuwaeleza maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Watanzania hao nao wamekuwa na jadi ya kumsomea risala, kumuuliza
maswali kwa nia ya kupata ufafanuzi wa masuala muhimu na kumpa Zawadi za
aina mbalimbali.
Rais Kikwete yuko katika ziara ya kikazi ya kuishukuru Nchi ya Uholanzi
kwa misaada ya kimaendeleo na pia kuiomba iendelee kuisaidia Tanzania ili
iweze kukamilisha na kuendeleza juhudi za kujenga na kuimarisha uchumi kwa
nia ya kuleta maendeleo Tanzania.
Rais Kikwete amepata fursa ya kuwaeleza Watanzania kuhusu uchaguzi
Mkuu ujao ambao ameahidi kuwa utasimamiwa vizuri ili Watanzania wapate
nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Rais pia amewaeleza Watanzania kuhusu juhudi mbalimbali za
maendeleo ambazo amezifanya katika kipindi cha utawala wake ambazo
zimechangia kukua kwa uchumi na Nchi kujijengea uwezo na kujiletea
maendeleo.
Rais ametumia fursa hiyo kuelezea jitihada zilizofanyika katika ujenzi wa
barabara, elimu, afya, maji na maendeleo katika teknolojia.
Rais Kikwete amemaliza ziara yake katika Nchi za Finland, Sweden na
Uholanzi na anatarajia kuondoka Uholanzi tarehe 9 Juni,2015 asubuhi na
kuwasili Dar es Salaam jioni.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
The Haque – Uholanzi.
9 Juni, 2015
Mheshimiwa Mkuu Rais JK umetika chicha sana baba hiko kiatu mzee naomba siku moja ufanye kama umevisahau nje msikitini wasela wako tujiokotee
ReplyDelete