Na mwandishi wetu.
Wazazi
wameaswa kuwa tayari kuwapokea Vijana au watoto wao walioamua kuacha matumizi
ya dawa za kulevya ili kuwalinda na vishawishi vinavyoweza kutoa nafasi ya kuwarejesha
tena kwenye matumizi ya Dawa hizo pamoja pombe haramu.
Mbunge wa
Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi ametoa wosia huo wakati wa kuwapokea
Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuacha kutumia Dawa za kulevya na
kupata mafunzo watakayoyatumia kuwasomesha wenzao kuachana na Dawa hizo hapo
katika Skuli ya Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “.
Balozi Seif
ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wapo Wazazi na
Familia Nchini ambao bado wanaendelea na tabia ya kuwatenga Vijana wao walioathirika
na Dawa za kulevya kwa kuchelea kufanyiwa matendo ya maudhi kama wizi.
Alisema
tabia hiyo inafaa kuachwa kwa vile kama haikutafutiwa ufumbuzi inaweza kuzalisha zaidi Vijana wanaotumbukia
katika matumizi ya Dawa za kulevya na hatimae kuwa na kundi kubwa la walevi ndani ya Jamii ambao ni nguvu kazi ya
Taifa.
Balozi Seif
alionyesha furaha yake kutokana na ujasiri
mkubwa ulioonyeshwa na vijana hao wa kuamuwa kuacha matumizi ya Dawa za
kulevya na kujitolea kuwa mfano kwa wenzao wenye tabia hiyo.
Wakati huo
huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif ameukabidhi Uongozi wa Mamlaka
ya Maji Zanzibar { ZAWA } shilingi Milioni 5,000,000/- kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kibanda
cha Maji katika Kijiji cha Kinduni.
Ujenzi wa
Kibanda hicho una lengo la kuimarisha miundo mbinu ya upatikanaji wa huduma za
Maji safi na Salama ndani ya Kijiji hicho chenye changamaoto ya upatikanaji wa
huduma hiyo muhimu.
Othman
Khamis Ame
Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif akisalimiana na mmoja kati ya Vijana sita walioamua kuachana na
matumizi ya Dawa za Kulevya katika Kijiji cha Fujano hapo katika Viunga vya vya
Skuli ya Fujoni. Kati kati yao ni Mwakilishi wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya
Dawa za kulevya na Pombe Tanzania Bwana
Abdulrahman Mohammed Abdulla.
Mwakilishi wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya
Dawa za kulevya na Pombe Tanzania Bwana
Abdulrahman Mohammed Abdulla akielezea mikakati ya taasisi yake katika
mapambano dhidi ya Dawa za kulevya hapa Nchini.
Balozi Seif akizungumza na baadhi ya Wananchi mara ya kukabidhiwa
Vijana Sita walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za kulevya waliokuwa
wakipata mafunzo kwenye Kituo cha Mombasa nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Kushoto ya
Balozi Seif ni Sheha wa Shehia ya Fujoni Bwana Said Mgeni Bakari na wa kwanza
kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “ Nd. Hilika Khamis
na Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi.
Kijana Ayoub Hussein Ayoub Mmoja kati ya Vijana sita walioamua mkuachana
na matumizi ya Dawa za kulevya akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake kuushukuru
uongozi wa Jimbo la Kitope kwa kusaidia mbinu na uwezeshaji uliowachangia wao
kuacha dawa hizo.
Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi shilingi Milioni 5,000,000/- Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Gharu hapo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa kibanda cha
maji katika kijiji cha Kinduni.
Dawa za kulevya zinavuruga maisha ya waathiriwa na jamaa zao, ni vizuri kusikia kwamba vijana wameacha hizi dawa.
ReplyDelete