Na Mwandishi wetu.
MABINGWA wa soka wa
Tanzania Bara, Yanga, Juni 27, mwaka huu wanatarajia kuvaana na SC Villa ya
Uganda katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
ukiwa na lengo la kukusanya fedha za kujengea kituo cha watoto wanaoishi kwenye
mazingira magumu na walemavu wa ngozi, yaani albino.
Akizungumza Dar es
Salaam jana katika ukumbi wa makao makuu ya Yanga yaliyopo Jangwani, jijini,
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Jonas Tiboroha, alisema kuwa katika mchezo huo
watachezesha kikosi chao kamili, kikiwajumuisha wachezaji wapya na nyota wa
zamani.
Alisema wameamua
kushiriki katika tamasha hilo kama sehemu ya kuonyesha jinsi wanavyoguswa na
jamii, ikiwa ni baada ya kuombwa kufanya hivyo na Taasisi ya Nyumbani Kwanza
Media kwani hata klabu kubwa Ulaya zimekuwa zikiafnya hivyo.
“Baada ya kuletewa wazo
hili na wenzetu wa Nyumbani Kwanza, tulikubaliana nao kwani ni zuri. Tumeona
klabu ya Yanga isipate isipate sifa kwa kutwaa ubingwa tu, bali pia hata
kufanya shughuli za kijamii kama hizi. Uongozi umebariki na hata Kocha Mkuu na
benchi lote la ufundi lina taarifa na ndio maana tumeanza mazoezi mapema
zaidi,” alisema.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Nyumbani Kwanza Media, Mossy Magere, alisema kuwa wazo
la kuandaa tamasha hilo lilikuja baada ya kutafakari ni vipi wanaweza kusaidia
makundi yenye mahitaji maalumu na wakaona ni vema kuishirikisha Yanga wakiwa
kama mabingwa wa Tanzania Bara.
“Mapato yatakayopatikana
yatafanya shughuli kusudiwa kwa kuanza rasmi ujenzi wa kituo huko Bagamoyo,
mkoani Pwani na tutakuwa tukifahamishana kila hatua ya mradi huo utakaogharimu
Sh bilioni 1.5 ambao tumepania uwe mfano wa kuigwa na wengine,” alisema Mossy.
Aliwapongeza Yanga
kwanza kwa kutwaa ubingwa wa Bara, lakini pia kukubali kushirikiana nao katika
kufanikisha tamasha hilo la aina yake.
Awali mechi hiyo ilikuwa
ichezwe kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, lakini kutokana na ushauri wa
Tiboroha, waliamua iwe Dar es Salaam ili kupunguza gharama za maandalizi yake,
hasa katika suala zima la usafiri kwa timu na mengineyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...