
Tulipokuwa skuli tulifundishwa kuwa, ili tuendelee tunahitaji mambo manne: Ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Jumuiya ya Wazanibari Waishio nchini Marekani (ZADIA) inauelewa fika umuhimu wa maneno hayo ya hekima, na ndio maana uongozi wake bora, kwa kutambua jukumu lake, daima umekuwa mbioni katika kutafuta na kubuni mbinu za kusaidia maendeleo nyumbani Zanzibar.
Kwa vile kuwa na watu tu haitoshi kuleta maendeleo ya nchi, ndio maana ZADIA imelipa kipaumbele swala la afya na ustawi wa jamii, kwani bila kuwa na watu wenye afya bora hatuwezi kufikia maendeo.
Kwa mantiki hiyo, kama ilivyoelezwa siku zilizopita, uongozi wa ZADIA ulifanya mawasiliano na Shirika la Pure Ultrasound la nchini Marekani na kufikia makubaliano ya kimsingi ya kuwapatia wataalamu wa Zaznzibar vifaa vya Ultrasound na mafunzo ya kuvitumia vifaa hivyo.
Na kama inavyokumbukwa, ujumbe wa shirika hilo tayari umeshatembelea Zanzibar katika hatua za awali za kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuisadia Zanzibar katika uwanja huo.
Katika kufuatilia hatua za utekelezaji wa makubaliano hayo, Mwenyekiti wa ZADIA Bwana Omar Haji Ali, kwa mara nyengine alikutana na uongozi wa Pure Ultrasound mnamo tarehe 18 Mei, 2015.
Katika mkutano huo, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa Pure Ultrasound itatuma mtaalamu wake wa ngazi za juu Visiwani Zanzibar mara tu baada ya kumalizika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mtalaamu huyo atakaa Zanzibar kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja kwa ajili ya kufanya utafiti wa kimkakati kuhusu mahitaji ya vifaa vya tiba katika hospitali za Zanzibar, pamoja na mafunzo yanayohitajika kwa wataalamu wetu katika fani hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...