Wakati umefika sasa kwa Dunia kujikita zaidi katika kukabiliana na migogoro isiyokwisha kwenye baadhi ya Mataifa inayozaa makundi ya wakimbizi kutokana na vita vinavyosababishwa na ukabila na mfumo mbaya wa siasa unaozalisha wanawake wajane na watoto yatima na kuwafanya kukosa haki zao za msingi za kibinaadamu katika kuishi maisha ya salama na furaha. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akiufungua Mkutano wa Kimataifa wa siku Mbili juu ya kukuza amani na maendeleo endelevu unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort nje kidogo ya Mjini Zanzibar na kuhuduriwa na Viongozi kadhaa wastaafu Barani Afrika wakiwemo pia wafanyabiashara maarufu. 
Dr. Shein ambae Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Dunia imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la akina Mama na Watoto walemavu wasio na hatia hasa katika Bara la Afrika wanaoendelea kuteseka kwenye kambi za wakimbizi kutokana na Nchi zao kukosa utulivu wa Kisiasa uliosababishwa na mapigano yasiyokwisha. Alisema mfumko huu wa wakimbizi usipotafutiwa mbinu za kudhibitiwa mapema kwa kuandaliwa mazungumzo ya kusaka suluhu kati ya makundi yanayohitilafiana kutatua matatizo yanayojitokeza upo uwezekano mkubwa wa kuzalisha utitiri wa umaskini kwenye mataifa yaliyokumbwa na vita. Rais wa Zanzibar alizitolea mfano Nchi zilizokumbwa na vita vya muda mrefu za Sudan, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi na Somalia ambazo Wananchi wao waliokimbia vita hivi sasa wengi kati yao wanaishi vilema pamoja na kukumbwa na umaskini uliopindukia mapaka. 
Mapema Mwenyekiti wa Mkutano huo wa kujadili Amani na Maendeleo endelevu Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Aman Abeid Karume alisema Mataifa ya Bara la Afrika bado yana wajibu wa kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi wake hasa wakimbizi. Dr. Karume alisema ushirikiano huo uende sambamba na ushirikishwaji wa makundi ya Kidini yanayoonekana kuwa na nguvu katika Jamii jambo ambalo yakitumika vyema yanaweza kuwaongoza wafuasi wake kujiepusha na vishawishi vinavyozaa migogoro ya kisiasa na kikabila. Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Richard Zezibera alisema Zanzibar itaendelea kuheshimika kama kituo cha Taaluma katika masuala ya kukabiliana na migogoro ya kisiasa na kikabila Duniani.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Nne kutoka kushoto akiwa pamoja na Viongozi wastaafu wa Afrika kabla ya Kuufungua Mkutano wa Kimataifa wa siku mbili wa amani na Maendeleo endelevu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Shein hapo Zanzibar Beach Resort Mazizini.Wa mwanzo kutoka kushoto ni Waziri kuu Mstaafuwa Kenya Bwa Raila Odinga, Rais Mstaafu wa Zanzibar Bw. Rupiah Banda na Rais Mstaafu wa Zanzibar ambae ndie mwenyekiti wa Mkutano huo Dr. Amani Abeid Karume.
 Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Richard Sezibera akitoa salamu za Umoja huo kwenye Mkutano wa Amani na Maendeleo endelevu.
 Mwakilishi wa Taasisi ya Global Peace Foundation Bwana James Amber akitoa salamu za Taasisi hiyo katika Mkutano wa Siku mbili kuhusu masuala ya Amani na Maendeleo endelevu.
 Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Bwana Raila Odinga akizungumza katika Mkutano wa siku mbili wa Amani na Mendeleo endelevu hapo Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akiufunguwa Mkutano wa siku mbili wa amani na maendeleo endelevu unaofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
 Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa siku mbili wa amani na maendeleo endelevu unaofanyika chini ya Mwenyekiti wake Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Abeid Karume. Picha na OPMR, ZNZ.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...