Kampuni
ya ujenzi ya CRJE kutoka China imekanusha vikali kuhusika na jengo la ghorofa
lililoporomoka katika makutano ya mitaa ya Indira Gandhi na Asia jijini Dar es
Salaam mwezi Machi mwaka 2013.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jijini Dar es Salaam
jana, inaeleza kuwa kampuni hiyo haikuwahi kushiriki katika ujenzi wa jengo
hilo lililoanguka.
“Tumesikitishwa sana na taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja la wiki inayoeleza kuwa kampuni yetu ilikua mkandarasi wa
jengo lililoporomoka. Hatujawahi kuhusika kwa namna yoyote na ujenzi wa jengo
lile,” Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Bw. Hu Bo alisema.
Aidha, kampuni hiyo ilieleza kuwa haijawahi kupewa kazi ya
kubomoa jengo hilo. Watu kadhaa walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika
ajali hiyo. Hata hivyo, Bw. Hu alisema kuwa kampuni yake ilishiriki katika
shughuli za uokoaji kwa misingi ya kibinadamu.
Alisema kuwa juhudi za kampuni hiyo zilitambulika na kampuni
ilizawadiwa cheti cha shukrani kutoka kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
CRJE imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini
Tanzania tangu mwaka 1970 na imepokea tuzo ya mkandarasi
bora wa kigeni mara tatu. Kampuni hiyo imeshiriki katika
ujenzi wa miradi mikubwa nchini kote ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya TAZARA, ujenzi wa hoteli
ya Kilimanjaro Hyatt Regency jijini Dar es Salaam na ujenzi
wa jengo la Bunge mjini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...