Waendesha bodaboda mkoani Mbeya wakiwa
katika maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa CCM Iromba kwenye uzinduzi wa mradi
wa kuwasajili na kuwapatia sare maalumu za kuwatumbua.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mh. Nyerembe Mnase
akihutubia hadhira kubwa ya waendesha bodaboda katika uzinduzi wa mradi wa
kuwasajili katika mfumo wa kumbumbuku pamoja na kuwapatia sare maalumu.
Meneja wa Kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom kanda ya Nyasa Bw. Minja akitoa salam za kampuni hiyo kama mdhamini wa
mradi wa kuwasajili waendesha bodaboda katika mfumo maalumu wa kumbukumbu.
Ule mchakato kabambe wa kuwasajili waendesha bodaboda katika mfumo
maalum wa kumbukumbu (database) na kuwakabidhi sare umeendelea kushika kasi
ambapo wakati utekelezaji ukiendelea jijini Dar es salaam, mwishoni mwa wiki
iliyopita uzinduzi wa mradi huo umefanyika kwa mbwembwe kubwa jijini Mbeya
ambapo maelfu ya waendesha bodaboda jijini humo walijitokeza kwa shamrashamra
tele kuuzindua mradi huo.
Uzinduzi huo wa aina yake uliofanyika
katika Uwanja wa CCM Iromba jijini Mbeya, ni mwendelezo wa mchakato unaofanywa
na kampuni ya mawasiliano, masoko na matangazo ya Alternative Communication ya
jijini Dar es Salaam, ikishirikiana na jeshi la polisi na kudhaminiwa na
kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, lengo likiwa kuwasaidia waendesha
bodaboda na abiria wanaotumia usafiri huo kutambulika kwa urahisi inapotokea
wamehusika katika matukio ya kihalifu.
Akiuzindua mradi huo mgeni rasmi katika
tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mh. Nyerembe Mnase, aliwapongeza waendesha
bodaboda hao kwa namna walivyoupokea mradi huo, na ameuagiza uongozi wa
Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuakikisha wanawapa chama cha UWABOM chumba kimoja
cha ofisi katika soko jipya la kimataifa la Mwanjelwa, na kwamba mradi wa
kuwatambua bodaboda utausaidia uongozi wa jiji kupata takwimu sahihi, wakati
ambapo jiji hilo linaandaa mkakati wa kuwatafutia eneo la viwanja vya ujenzi
kwa ajili ya waendesha bodaboda.
“Kwa hatua mliyofikia, tutawatafutia eneo
la viwanja vya ujenzi ili muendelee zaidi kwa kuwa na makazi bora. Lakini
nawasisitiza muendelee kuwa watii wa sheria barabarani, na kuwafichua wale
wasio waaminifu wanaoshiriki katika vitendo vya kihalifu nyuma ya mgongo wa
bodaboda.” Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji wa
Alternative Communication Bw. Edward Mgaya, aliwamwagia sifa waendesha bodaboda
wa mkoani Mbeya kwa namna walivyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuutekeleza mradi
huo, hadi kufikia hatua ya kufungua SACCOS ya wanachama wa Chama cha Wamiliki
na Waendesha Bodaboda na Bajaj mkoani humo (UWABOM).
Naye Katibu wa UWABOM Bw. Msumba Mdesa,
katika risala kwa mgeni rasmi, uliushukuru mradi huo wa kuwasajili na kupewa
sare, na kuongeza kuwa sare hizo zimewafanya wafanikiwe kujenga mshikamano
wenye nia ya kujikwamua kwenye janga la umasiki, na wanachama kuwa na nidhamu
ya hali ya juu katika kutii sheria bila shuruti.
Mradi wa kuwasajili waendesha bodaboda na
kuwapatia sare maalum umekuja kufuatia madai kuwa baadhi yawaendesha bodaboda
wasio kuwa waaminifu hujihusisha katika matukio ya kihalifu au kutumiwa na
wahalifu kuvunja amani na kupotea bila ya kutambulika.
Kupitia mradi huu waendesha bodaboda
waliosajiliwa pia watapata faida ya kupewa huduma ya bima ya afya, mafunzo ya
usalama barabarani na Ujasiriamali, huku
kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambayo ndio wadhamini wa mradi, ikiwa
imewatengea bodaboda kifurushi maalumu cha simu ambacho kina dakika 30 za
maongezi, sms 500 na mb 100 za intanet kwa gharama ya shilingi 500 tu, na
kikidumu kwa muda wa mwezi mmoja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...