![]() | |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizindua uvunaji wa matikiti maji kwa wakulima wa shehia ya Donge Muwanda. |
![]() | ||||
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizindua uvunaji wa matikiti maji kwa wakulima wa shehia ya Donge Muwanda. |
![]() | |
Mkulima wa matikiti maji na pilipili boga Bw. Salum Khamis Kiregu akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhusiana na changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho. |
Na:
Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu juhudi zinazochukuliwa
na wananchi wa Donge katika kuendeleza kilimo cha matunda na mboga mboga.
Amesema iwapo kilimo
hicho kitawekeza mikakati imara, kinaweza kuwa mkombozi wa kweli kwa wakulima
na kuweza kuweza kuongeza kipato chao.
Maalim Seif ameeleza
hayo wakati akizindua uvunaji wa matikiti maji na pilipili boga katika shehia
za Donge mchangani na Muwanda katika Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.
Amesema katika siku
za hivi karibuni, kilimo hicho kimepata mafanikio makubwa na kupunguza
uagiziaji wa bidhaa hizo nje ya Zanzibar kutoka asilimia 80 hadi asilimia 20.
Amefahamisha kuwa
lengo la Serikali ni kuimarisha zaidi kilimo cha matunda na mboga mboga ili
kuweza kukidhi soko la ndani na kuacha kuagizia bidhaa hizo kutoka nje ya
Zanzibar.
Amesema
kinachohitajika hivi sasa ni kwa Serikali kuongeza mashirikiano na wakulima,
ili kusaidia kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa
maji pamoja na pembejeo.
Makamu huyo wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar ameiagiza Wizara ya Kilimo kupeleka mabwana na mabibi
shamba wa kutosha katika shehia hizo za Mchangani na Muwanda, ili kusaidia
utaalamu kwa wakulima hao na kuweza kuzalisha zaidi.
Nae Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Bw. Affan Othman Maalim, amesema tayari
Serikali imeanza kufanya utafiti kujua maeneo ya kuchimba visima ili kuwasaidia
wakulima hao kuondokana na tatizo la upungufu wa maji.
Hata hivyo
amewashauri wakulima hao kujikusanya pamoja ili kurahisisha miundombinu ya maji
kuweza kuwafikia walengwa.
Kuhusu tatizo la
pembejeo, Bw. Affan amesema Wizara ya Kilimo inaandaa utaratibu wa kulipeleka
suala hilo katika ngazi za juu, ili kuwawezesha wakulima wa matunda na mboga
mboga kuweza kupatiwa ruzuku za pembejeo za kilimo kama wanavyopatiwa wakulima
wa mpunga.
Mapema mmoja kati ya
wakulima hao Bw. Salum Khamis Kiregu, amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa
licha ya mafanikio wanayoyapata, bado wanakabiliwa na tatizo la soko la kuuzia
bidhaa hizo, na kuiomba serikali kuandaa mazingira bora ya soko kwa wakulima
hao.
Amesema hivi sasa
wanalazimika kuuza bidhaa zao kwa bei ya chini kupitia kwa wafanyabiashara,
jambo ambalo limekuwa likipunguza kipato chao licha ya kuzalisha bidhaa hizo
kwa wingi.
Bw.
Kiregu ameeleza matatizo mengine yanayowakabili kuwa ni pamoja wadudu
waharibifu na maradhi ya mimea, na kuwaomba wataalamu wa kilimo kuwa karibu na
wakulima ili kusaidia kukabiliana na changamoto hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...