Na Grace Michael
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekutana na Uongozi wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) kwa
lengo la kubadilishana uzoefu na changamoto katika suala la utambuzi wa watumiaji wa huduma za
vitambulisho.
Hatua hiyo ya NHIF kukutana na uongozi huo inakusudia kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa
wanachama wake ambao tayari wana vitambulisho vya Taifa.
Akizungumzia hatua hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa NHIF Bw. Michael Mhando, amesema Mfuko wake
umeona kuna umuhimu mkubwa wa kuunganisha nguvu na rasilimali chache zilizopo katika eneo
hilo kwa manufaa ya wote.
“Tumeona ni vyema tutakakutana na wenzetu wa NIDA ili kuona ni kwa namna gani tunaweza
kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama wetu kupitia vitambulisho vya Taifa lakini pia
kubadilishana uzoefu katika uandaaji wa vitambulisho ambavyo ni vya kisasa zaidi,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Mifumo Habari wa NHIF, Bw. Ali Othman amesema kuwa hatua hiyo ni fursa
kubwa kutokana na ukweli kwamba kitambulisho cha Taifav kitamuwezesha mwananchi kutumia
huduma mbalimbali.
“Kitambulisho cha Taifa kinajibu nani ni nani, anakaa wapi, anamiliki nini na anafanya nini taarifa
ambazo ni za muhimu sana katika kuuwezesha Mfuko kutambua kila kundi na namna ya
kuhamasisha kuwa na Mfumo wa bima ya afya kulingana na kundi husika,” anasema.
Ametumia mwanya huo kuushukuru uongozi wa NIDA KWA KUUSHIRIKISHA Mfuko katika hatua za
awali za uandaaji na ubunifu wa vitambulisho vya Taifa jambo ambalo litarahisisha sana utekelezaji
wa hatua hii ya sasa.
Bw. Othman amesema kuwa kwa kutumia teknolojia ya Mifumo Habari kuna uwezekano mkubwa
wa wanachama wa NHIF kutumia vitambulisho vya Taifa sanjari na NHIF katika upatikanaji wa
huduma ikiwemo udhibiti wa mianya ya udanganyifu hivyo Mfuko unatarajia kwa kila hali kuanza
kutumia vitambulisho vya NIDA katika utambuzi wa wanachama wake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...