Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Thomas Samkyi, (pichani kati) akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Benki hiyo,Kinondoni kuhusu uzinduzi wa benki hiyo utakaofanyika Agosti 7, 2015,jijini Dar . Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Sera, Bwana Francis Assenga, na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki, Bi Rosebud Violet Kurwijila.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Bi Rosebud Violet Kurwijila akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani),katika ofisi za Benki hiyo jijini Dar mapema leo kuhusu uzinduzi wa benki hiyo. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki Thomas Samkyi, na Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Sera, Bwana Francis Assenga.
Baadhi ya Wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo mapema asubuhi ya leo

 Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuzindua rasmi benki ya kwanza ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, ambayo inalenga kuanzisha mtizamo mpya wa kukiendeleza kilimo kupitia kushirikisha wadau mbali mbali, kuangalia kila mnyororo wa thamani kwa ukamilifu wake, pamoja na kuwa na ubunifu katika kuchangia kifedha kwenye miradi ya muda mrefu, ya kati na muda mfupi kwenye sekta ya kilimo. Benki hiyo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa sekta ya kilimo ambayo imeajiri zaidi ya aslimia 70 ya Watanzania.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika kwa ngazi mbili: ngazi ya kwanza itahusisha uzinduzi wa Makao Makuu ya TADB jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 7 ya mwezi huu; ambapo ngazi ya pili itahusisha uzinduzi rasmi wa TADB mbele ya wadau wake wakuu ambao ni Wakulima, kwenye Maonesho ya Nane Nane Mkoani Lindi, katika kilele cha Siku Kuu ya Wakulima hapo tarehe 8 Agosti 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya benki hiyo yaliyoko Barabara ya Kinondoni, Mkurugenzi Mkuu wa benki, Bwana Thomas Samkyi, alisema dhumuni kuu la uanzishaji wa benki hiyo ni kuboresha tija katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo kwa kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali ili kuwezesha uendelezaji wa miundombinu ya kilimo kama miradi ya umwagiliaji, usafirishaji, uhifadhi, mindombinu ya masoko, n.k. ambayo inachangia maendeleo ya sekta ya kilimo.

‘Uanzishwaji wa benki hii unalenga kuziba mianya mikubwa ya ukopeshaji kwenye kilimo ambayo inaachwa na benki za biashara, ili kuchochea kukua kwa sekta ya kilimo, kwa kutoa mikopo na huduma nyingizezo za uwezeshaji wa kilimo kwa wakulima, ambao wengi wao hawana uwezo wa kupata huduma za kibenki’ alisema Bw. Samkyi.

Akieleza zaidi kuhusu uanzishwaji wa benki hiyo, Bwana Samkyi alisema Benki ya Wakulima itakuwa msitari wa mbele katika kusukuma shughuli za kilimo pamoja na kuchagiza benki na taasisi nyingine za kifedha kushiriki katika kuwezesha shughuli za kilimo.

‘Benki hii imeundwa ili kutoa mikopo kwa masharti nafuu, pamoja na kutoa huduma nyinginezo zitakazoongeza uwezo wa wakulima kukopa na kuzalisha. Ili kufanikisha haya, benki inabidi iwe na vyanzo endelevu vya fedha za kutosha kwani nchi hii ni kubwa na wadau wa benki ni wengi sana. Lengo kuu ni kubadili kilimo cha Tanzania kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara’ alisema Bw. Samkyi.

Benki hii pia inatarajiwa kuwa ni kiungo muhimu cha utekelezaji wa mageuzi ya awamu ya pili ya sekta ya kifedha, na vile vile kuboresha maendeleo ya kilimo nchini ikizingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 pamoja na mipango mbalimbali ya maendeleo ya miaka mitano mitano, Mkakati wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo, na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA), pamoja na sera mbali mbali za Serikali zinazohusu sekta ya kilimo.
  
Kuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania

Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (katika kuanzishwa kwake) ni taasisi mpya ya kifedha iliyoanzishwa na serikali kwa madhumuni ya kuboresha huduma za kifedha ikiwa ni pamoja na huduma nyinginezo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Benki hii imeanzishwa ili kufikia malengo ya taifa yaliyoafikiwa katika Tanzania Vision 2025, kusudio likiwa ni kuwezesha na kutosheleza upatikanaji wa chakula, kuchochea kilimo cha biashara, pamoja na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umasikini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...