Mkurugenzi
wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati
na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo (Kulia), akimwongoza Kaimu Katibu Mkuu
wa Wizara, Mhandisi Ngosi Mwihava kuingia Ukumbi wa Semina ya Wathamini Madini
ya Vito na Almasi nchini, iliyofanyika Agosti 12 na 13 katika Hoteli ya Gold
Crest jijini Mwanza.
Kutoka
Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito
cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT) Archard Kalugendo, Kaimu Katibu Mkuu
wa Wizara Mhandisi Ngosi Mwihava, Kaimu Kamishna wa Madini nchini Mhandisi Ally
Samaje na Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu Mrimia Mchomvu, wakijadili
jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa Semina ya Wathamini Madini ya Vito na
Almasi nchini, iliyofanyika Agosti 12 na 13, 2015 katika Hoteli ya Gold Crest
jijini Mwanza.
Meza
Kuu – wakiwa katika Semina ya Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini. Semina
ilifanyika Agosti 12 na 13, 2015 katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza. Kutoka
Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito
cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo, Kaimu Katibu Mkuu
wa Wizara Mhandisi Ngosi Mwihava, Kaimu Kamishna wa Madini Ally Samaje na
Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu Mrimia Mchomvu.
WATHAMINI MADINI VITO WAASWA KUWA WABUNIFU
Na Veronica Simba - Mwanza
Kaimu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava amewataka Wathamini
Madini ya Vito na Almasi nchini kuendelea kuwa wabunifu ili kutafuta majibu na
suluhisho kwa changamoto zinazoikabili tasnia ya vito nchini.
Aliyasema hayo
alipokuwa akifungua Semina ya Nne ya Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini
iliyofanyika Agosti 12 na 13, mwaka huu katika Ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest,
jijini Mwanza.
Mwihava
alisema kuwa changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hiyo zitaweza
kuondolewa endapo watumishi katika kada hiyo watajituma kufanya kazi kwa
uaminifu, weledi na ubunifu wa hali juu. “Napenda
kuwakumbusha kwamba Watanzania wanataka kuona faida stahiki kutoka katika sekta
ya madini hasa itokanayo na almasi na vito vingine; kadhalika hata mimi nataka kuona
matokeo yanayopimika na malengo hayo kutimia na hata kuzidi viwango wanavyotarajia,”
alisema Kaimu Katibu Mkuu.
Akifafanua
zaidi, Mwihava aliongeza kuwa angependa kuona Soko la uhakika kwa Madini
yanayopatikana nchini hususan Almasi na Vito ili Watanzania wanaojishughulisha
na biashara hiyo wajue utaratibu wote.
Alisema kuwa
angependa kuona wataalam hao wakitumia ipasavyo mitandao iliyopo katika
kuwavutia wafanyabiashara na wakataji wa vito kuja nchini kununua na kuwekeza
katika tasnia husika.
Aidha, Mwihava
aliongeza kuwa angependa kuona wataalamu hao wa Madini ya vito na almasi
wakitumia ujuzi wao katika kuwasaidia wadau wa tasnia husika kupata tafsiri
sahihi na kuzingatia Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na Kanuni zake.
“Nawaagiza
mzingatie maadili na miongozo ya kazi katika utekelezaji wa majukumu yenu;
msome na kuzingatia Sera ya Madini ya mwaka 2009, Sheria ya Madini ya mwaka 2010
pamoja na kanuni zake na Mkataba wa Huduma kwa Mteja,” alisisitiza Mwihava.
Vilevile,
Kaimu Katibu Mkuu alitahadharisha kuwa yeyote atakayefanya kazi kinyume na
matarajio, kwa kupokea rushwa, wizi au kufanya jambo jingine lolote kinyume na
maadili ya utumishi wa Umma na kusababisha kuathiri juhudi zinazofanywa na
Wizara, hatavumiliwa.
Akizungumzia
mchango wa Serikali katika kuinua tasnia ya Madini ya vito na almasi, Mwihava
alisema Wizara imeahidi kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya madini ili
kuongeza uwezo kwa Serikali kujitegemea katika bajeti yake.
“Endapo azma
hii itafanikiwa, uchumi wetu kama Taifa utakua, fursa za ajira zitaongezeka na
kipato cha Watumishi kitaboreshwa. Aidha, wananchi watapata huduma stahiki,
muingiliano wa biashara utakua na hivyo kuchochea ufikiaji wa malengo ya Dira
ya Taifa, yaani kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo 2025.”
Alisisitiza
kuwa suala muhimu zaidi ni kuhakikisha Watanzania wanaridhishwa na utendaji
kazi wa watumishi wa Serikali hususan walioko katika kada husika na kuwaonyesha
Watanzania kwamba wana uwezo wa kusimamia sekta husika kwa niaba yao na pia wananchi
waone kwa maneno na vitendo kwamba kazi hiyo inafanyika vizuri.
Mwihava
alihitimisha kwa kuwataka washiriki wa semina hiyo kuitumia kama fursa muhimu
ya kujitathmini, kubadilishana uzoefu, kupeana mbinu za utendaji bora, kutafuta
majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili na kukumbushana maadili mema ya
kazi na utumishi wa umma.
Alitoa
changamoto kuwa anatarajia baada ya semina husika, wataalam hao wa sekta ya
Madini vito na almasi watakuja na mkakati wa kuboresha ukusanyaji mapato ya
Serikali kutoka katika tasnia ya almasi na vito, ili kuisadia Wizara kufikia
malengo ya makusanyo na kuboresha utendaji wao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...