Katibu Mdogo wa Ubalozi wa Japan, Noriko TANAKA (kulia) akipokea kitabu cha wageni kutoka kwa Mratibu wa kata ya Segese iliyopo halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Bi. Victoria Maige alipofikia katika ofisi hizo kwa ajili ya zoezi la kusaini kitabu cha wageni kabla ya kuelekea kwenye mahafali ya Mpango wa Elimu Mbadala kwa Wasichana walioacha shule kwa sababu za Ujauzito unaofadhili Ubalozi wa Japan na kuratibiwa na UNESCO.
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
WAZAZI wenye umri mdogo 149 mkoani Shinyanga ambao walipata mimba wakiwa shuleni wamekamilisha mafunzo ya miaka miwili ya stadi mbalimbali za maisha mkoani hapa.
Wazazi hao wenye umri mdogo ni miongoni mwa wazazi 220 walioanza mafunzo hayo miaka miwili iliyopita chini ya mradi wa Elimu Mbadala kwa Wasichana walioacha shule kwa sababu za Ujauzito unaofadhiliwa na Ubalozi wa Japan na kuratibiwa na UNESCO.
Wazazi hao vijana kutoka wilaya tatu za mkoa wa Shinyanga za halmashauri ya Shinyanga, Msalala na Kahama walikuwa wanajifunza katika vituo 10.
Wengine walishindwa kuhitimisha mafunzo yao kwa sababu tofauti.
Pamoja na kumaliza mafunzo hayo na wengine kujiandaa kwa masomo ya sekondari, wanafunzi hao walijifunza shughuli mbalimbali ambazo zinawawezesha kujiajiri na kuongeza kipato kwa familia zao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Msalala, Vivian Masangya alisema pamoja na akimama wadogo hao wengine walishindwa kukamilisha masomo yao kutokana na utoro uliosababishwa na familia, umbali wa vituo husika na wawezeshaji kuwa na posho ndogo ya kuwezesha mafunzo kumekuwepo na mafanikio makubwa.
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Elimu ya Watu Wazima MOEVT, Salum Mjagila (kulia) akisaini kitabu cha wageni katika ofisi za kata ya Segese iliyopo halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama mara baada ya kuwasili katika ofisi hizo. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu wa Wazima nchini, Dk. Fidelis Mafuniko na kushoto ni Mratibu wa kata ya Segese iliyopo halmashauri ya Msalala, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, Bi. Victoria Maige.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...