Mkimbizi kutoka nchini Burundi, Jacqueline Elulu (mwenye
mtoto), akisubiri kupata huduma ya afya katika kituo cha Red Cross kinachotoa
huduma za afya kwa wakimbizi walioko katika kambi ya Nyarugusu iliyoko wilayani
Kasulu mkoani Kigoma. Shirika la Red Cross ni mojawapo ya wadau wanaoshirikiana
na Serikali kutoa huduma za afya katika kambi ya Nyarugusu.
Mkimbizi kutoka Burundi akipata huduma ya maji katika moja
ya vituo vya maji vilivyojengwa katika Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. Huduma za maji safi na salama ni mojawapo ya
mambo yanayotiliwa mkazo ili kulinda afya za wakimbizi.
Wakimbizi kutoka nchini Burundi walioko katika kambi ya Nyarugusu wakiwa
wamebeba shehena ya unga wa mahindi jana, muda mfupi baada ya kugawiwa chakula
hicho Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia chakula (WFP), lililoweka
kituo chake katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu, mkoani
Kigoma.
PICHA ZOTE NA KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA
NDANI YA NCHI.\
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCH
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
IDADI YA WAKIMBIZI WA BURUNDI WANAOHIFADHIWA KATIKA KAMBI YA WAKIMBIZI
YA NYARUGUSU YAONGEZEKA
Idadi ya wakimbizi kutoka Burundi wanaokimbia nchi yao na kuingia
nchini Tanzania imefikia 91,661 kwa takwimu za Jumanne, tarehe 08 Septemba,
2015. Wakimbizi hawa kwa sasa
wamehifadhiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu
mkoani Kigoma.
Tangu waanze kuingia mwezi Aprili mwaka huu, Wizara ya Mambo
ya Ndani ya nchi kwa kushirikiana na
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine
imekuwa ikiwapokea na kuwapa hifadhi na huduma nyingine muhimu. Huduma hizi ni pamoja na za ulinzi, chakula,
maji, elimu na afya.
Kutokana na kuboreshwa kwa huduma za ulinzi, hali ya ulinzi
na usalama katika kambi ya Nyarugusu na maeneo yanayoizunguka imeimarika ambapo
upo usalama wa kutosha. Kazi hii inafanywa na Polisi kwa kushirikiana na
vikundi vya ulinzi shirikishi vinavyojumuisha baadhi ya wakimbizi wanaoishi
katika kambi hii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...