Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na kiongozi wa Ujerumani Kansela Angela Merkel kwenye ubalozi wa kudumu wa Ujerumani Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Ijumaa jioni.Rais Kikwete yupo katika ziara ya kikazi nchini Marekani ambapo mbali na kukutana na wadau wa Maendeleo anatarajiwa kutoa hotuba yake katika kikao cha 70 cha Baraza Kuu la Umioja wa Mataifa(UN General Assembly
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na kiongozi wa Ujerumani Kansela Angela Merkel kwenye ubalozi wa kudumu wa Ujerumani Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Ijumaa. Picha na Freddy Maro.
------------------------------------
JK:
Kampeni zinaendeshwa kwa uhuru wa kumwaga kabisa
·
Afafanua
kuwa Tanzania inataka mchakato utakaozaa uchaguzi huru na wa haki
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa, Septemba
25, 2015 amemwambia Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Angela Merkel kuwa upo uhuru
mkubwa na usiokuwa kifani kwa vyama vyote ya siasa kufanya kampeni zake kwa
ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Aidha, Rais Kikwete
amemwambia Kansela Merkel kuwa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani linalotafuta
kufanya mapendekezo ya jinsi dunia inavyoweza kujiandaa vizuri zaidi kwa
magonjwa ya milipuko, sasa linakaribia kumaliza kazi yake na lipo katika hatua
ya kuandaa mapendekezo kuhusu nini dunia ifanye katika siku zijazo.
Rais Kikwete
amekutana na kuzungumza na Kansela Merkel katika mkutano uliofanyika kwenye
Ubalozi wa Ujerumani kwenye Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York na kuombwa na
Mama Merkel mwenyewe. Viongozi hao wawili wapo New York, Marekani kuhudhuria
shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (United Nations General
Assembly (UNGA).
Katika mazungumzo
hayo, Kansela Merkel alitaka kujua kutoka kwa Rais Kikwete kuhusu mwenendo
mzima wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea nchini na uhuru unaotolewa kwa
kila chama kufanya kampeni zake.
“ Kama unavyojua Mheshimiwa
Kansela tuko katikati ya Kampeni ya Uchaguzi Mkuu. Kampeni zinakwenda vizuri.
Tunao wagombea wa urais nadhani kiasi cha wanane hivi na kila chama kinaendesha
kampeni zake kwa uhuru mkubwa na usiokuwa na kifani. Tunataka mchakato ambao
utazaa uchaguzi huru na wa haki na hivyo ni muhimu kwa kila chama kuendesha
shughuli zake za kampeni kwa uhuru,” Rais Kikwete amemwambia Mama Merkel.
Rais pia amemwambia
Kansela Merkel kuhusu baadhi ya mambo makubwa ya kampeni yakiwemo mambo
yanayohusu masuala ya huduma za kijamii kama vile afya, elimu na mapambano
dhidi ya umasikini. “Kampeni zote kwenye ngazi zote – ngazi ya urais, ngazi za
wabunge na ngazi za Serikali za mitaa zinakwenda vizuri kwa uhuru wa kumwaga
kabisa.”
Rais Kikwete pia
ametumia mkutano wake na Kansela Merkel kumweleza Mama huyo kuhusu kazi ya Jopo
ya Watu Mashuhuri Duniani kuhusu Matatizo ya Afya akisisitiza kuwa baada ya
hatua ya kuwasilikiza watu mbali mbali, sasa Jopo limeanza kuandaa maoni yake
na mapendekezo.
Jopo hilo ambalo
liliteuliwa Aprili mwaka huu na Katibu Mkuu wa UN Mheshimiwa Ban Ki Moon
kufuatia majonzi makubwa yaliyosababishwa na ugonjwa wa Ebola katika nchi za
Guinea, Liberia na Sierra Leone, linatarajiwa kukabidhi ripoti yake kwa
Mheshimiwa Ban Ki Moon Desemba mwaka huu.
Ujerumani ni moja ya
nchi zinazoongoza dunia katika kuunga mkono na kugharimia shughuli za Jopo hilo
na pia imewekeza fedha nyingi katika kugharimia uboreshaji wa mifumo ya afya
katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Baadaye usiku, Rais
Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi wa nchi nane duniani ambao wamehudhuria
chakula cha usiku ambacho kimeandaliwa na Kansela Merkel kwa ajili ya viongozi
ambao wanaunda kundi la nchi ambazo zimekubali kubeba wajibu wa kuhakikisha
utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals
–SDG) ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG)
ambayo muda wake wa utekelezaji wa miaka 15 umemalizika.
Tunashukuru sana kwa ujumbe, ila huyu mama sio kansela ni chansela..... Kuna tofauti kubwa
ReplyDeleteMtoa Anony namba 1 tunashukuru kwa kurekebisha lakini mbona wasomaji tumemuelewa mwandishi kulikuwa hakuna haja ya kukosoa,je ? unaweza kutusaidia kwa kiswahili maana yake nini?
ReplyDeletewadau
FFU