Mama Salma Kikwete amesema kuwa vyama vya upinzani havina uwezo wa kutatua changamoto za maendeleo kwani havina ilani za uchaguzi ambazo ni mkataba baina ya wananchi na viongozi . 
Aliyasema hayo kwenye kata ya Pera Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni wa kumnadi mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete na diwani wa kata hiyo Lekapo Laini. 
Mama Salma alisema kuwa ilani ndiyo mkataba baina ya viongozi na wananchi juu ya kukabili changamoto walizonazo wananchi lakini vyama vya upinzanzani havina ilani hivyo ni vigumu kutatua kero zinazowakabili wananchi. 
“Viongozi wa vyama vya upinzani wanaoomba nafasi za uongozi hawana uwezo na hawana ilani juu ya utekelezaji wa namna ya kutatua changamoto za wale watakaowaongoza hivyo ahadi wanazotoa ni za uongo kwani watatekeleza kwa makubaliano yapi lakini CCM imetoa ilani kama dira ya kuongoza namna ya kuzikabili changamoto zilizopo,” alisema mama Salma Kikwete. 
Alisema kuwa makubaliano yao na wananchi hayapo kwani ilani ndiyo makubaliano ambayo yameandikwa kwa maandishi hivyo wale wanaosema watatekeleza ahadi bila ya kuonyesha mkataba ni waongo. 
“CCM katika miaka 38 tangu ilipoanza kuwatumikia wananchi imeonyesha mabadiliko makubwa kwa vitendo kwani ilani yake inatekelezeka ambapo ilani ya mwaka 2015 hadi 2020 inaonyesha itafanya nini katika kipindi cha miaka mitano lakini wapinzani hawana lolote hivyo nafasi ya Urais Dk John Magufuli, Ubunge Ridhiwnai Kikwete na diwani wa kata ya Pera naye wa CCM haina haja ya kuweka wapinzani,” alisema Mama Salma Kikwete. 
Kwa upande wake Ridhiwani Kikwete alisema kuwa mikakati yake endapo atachaguliwa kwa miaka mitano ijayo ni kuhakikisha kuwa ilani ya uchaguzi ya miaka mitano inatekelezeka kama ilivyosema ili kuwaondolea wananchi changamoto zilizopo. 
Ridhiwani alisema kuwa baadhi ya mambo ambayo atayasimamia ni kuhakikisha ujenzi wa zahanati kwenye vijiji vya Malivundo, Pingo na Pera ambako kuna changamoto ya ukosefu wa zahanati ambapo kwenye ilani inataka kila kijiji kiwe na zahanati na kituo cha afya kila kata. 
Naye mwenyekiti wa Wilaya ya Bagamoyo Almas Maskuzi alisema kuwa wao kama viongozi wa CCM ni kuhakikisha ahadi zinazotolewa na wagombea zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya miaka mitano ijayo.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia wakazi wa kata ya Pera Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, wakati wa kampeni za kuwania ubunge Jimbo hilo linalowaniwa na Mbunge wa CCM Ridhiwani Kikwete.
Mama Salma Kikwete akielezea jambo mbele ya mgombea wa CCM Ridhiwani Kikwete na kushoto mgombea udiwani kata ya Pera Lekapo Laini, wakati mkutano wa hadhara wa kumnadi mbunge wa Jimbo la Chalinze (Picha na John Gagarini)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...