
Tuzo hizo zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA zinatarajiwa kufanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo pia TASWA itatoa Tuzo ya Heshima kwa Rais Kikwete ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa sekta ya michezo katika uongozi wake.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Adam Akyoo, alisema wameamua kusaidiana na TASWA kwa sababu Rais Kikwete ni mdau mkubwa wa michezo na pia wa masuala ya utalii.
‘’Dk. Kikwete ni mdau mkubwa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwani kwa kipindi chote ambacho amekuwa Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ametembelea hifadhi hii mara nyingi zaidi kuliko viongozi wengine wote wa Taifa letu waliomtangulia.
‘’Pia amekuwa mdau muhimu na wa mstari wa mbele wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kutangaza vyema vivutio vya watalii vya hifadhi ya Ngorongoro katika mataifa mbalimbali duniani alikokwenda kwa ziara za kikazi.
‘’Jambo hili limeleta watalii wengi nchini kutoka mataifa mbalimbali dunini. Vile vile ziara zake za mapumziko hifadhini wakati wa sikukuu mbalimbali zimewahamasisha sana Watanzania walio wengi kutembelea hifadhi hii kutoka kote nchini na hata nchi jirani,’’ alisema Akyoo.
Pia alisema waandishi wa habari ni wadau wakubwa na muhimu katika harakati za utalii na ndiyo sababu wameamua kuisaidia TASWA ifanikishe shughuli yake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando aliishukuru mamlaka ya hifadhi hiyo na kusema kuwa msaada huo ni mkubwa na kuomba wadau wengine waungane nao kufanikisha jambo hilo.

Alisema TASWA imeamua kuandaa hafla ya wanamichezo kumuaga Rais na pia kumpa tuzo kwa vile wakati wa uongozi wake amefanya mambo makubwa katika sekta ya michezo.
Kwa mujibu wa Mhando, wanamichezo pia watatumia tuzo hizo zilizoandaliwa na TASWA kumuaga Rais Kikwete anayemaliza muda wake kikatiba baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 25, mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...