PATASHIKA ya michuano ya vijana chini ya miaka 12 ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa, imeendelea kutimua vumbi katika dimba la Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam, ambapo timu za Temeke na Mwanza zilipepetana kwa upande wa wasichana huku Mwanza na Morogoro walitifuana vikali kwa upande wa wavulana. 
Kwa kuanzia na mchezo ambao ulizikutanisha timu za wavulana, Mwanza waliwasambaratisha vibaya Morogoro kwa kuwashindilia magoli 3-1. Mwanza ambao walionekana kutakata kila idara, walijipatia bao la uongozi mnamo dakika ya 30 kupitia Lazaro Richard, baada ya kuitokea pasi nzuri iliyopigwa na David Richard na kumchambua vizuri kipa wa Morogoro kisha kuukwamisha mpira huo kimiani. 
 
Morogoro ambao katika mchezo wa Jumatatu wiki hii, waliitandika Kinondoni mabao 2-1, waliamka kutoka usingizi na kufanya mashambulizi kadhaa ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda. 

Alikuwa ni David Richard ambaye aliandikia Mwanza bao la pili mnamo dakika ya 54, kutokana na krosi safi iliyochongwa kutoka mashariki mwa uwanja na kuusindikiza kwa uzuri kabisa mpira huo langoni mwa Morogoro. 
Baada ya goli hilo, Morogoro waliamka na kupeleka mashambuliza ya mara kwa mara langoni mwa Mwanza, na ndipo mshambuliaji wao hatari Evidence Kiongozi alipofunga goli dakika ya 63 na kuamsha matumaini ya walau kusawazisha na hatimaye kutafuta goli la ushindi. Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa upande wa Morogoro, baada ya David Richard kwa mara nyingine tena, kuifungia Mwanza bao la tatu na mwisho katika mchezo huo mnamo dakika ya 68 na kuhitimisha karamu ya magoli kwa upande wa timu yake. Katika mchezo mwingine, wasichana wa Temeke waliwaadabisha vikali Mwanza kwa kuwafumua magoli 3-0.
Temeke ambao katika mchezo wao wa kwanza walitaoa kipigo cha mbwa mwizi cha magoli 8-0 dhdi ya Arusha, walianza kupata bao mnamo dakika ya 11 baada ya Shamimu Khamisi kufunga goli maridhawa, baada ya kutokea rapsha langoni mwa Mwanza na kuipa timu yake goli la uongozi. 

Iliwachukua takribani dakika takraibani 28, Temeke wakapata bao la pili kupitia kwa Rose Mpoma baada ya kuachia shuti kali la mbali na kuzama moja kwa moja wavuni, na kumwacha mlinda mlango wa Mwanza asijue la kufanya langoni mwake. Mpaka timu hizo zinakwenda mapumzikoni, Temeke walikuwa mbele kwa magoli 2-0. 
 Temeke waliendeleza kilio kwa wapinzani wao, katika kipindi cha pili kwa kushindilia msumari wa tatu na wa mwisho mnamo dakika ya 56, baada ya Oppah Masoud kugongeana mpira vizuri na Rose Mpoma na hatimaye kuusukumiza moja kwa moja mpira kimiani. 
Baada ya kupata goli la tatu, Temeke walionekana kuridhika na kucheza kwa kijiamini huku wakisubiri kipenga cha mwisho cha mwamuzi, huku wakiwa wamejikunyajia pointi tatu kibindoni.
Patashika ya michuano ya vijana chini ya miaka 12 ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa,
Patashika ya michuano ya vijana chini ya miaka 12 ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa baina ya Mwanza na Morogoro

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...