DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
wa
Tanzania na Marekani
·
Aiomba
Serikali ya Marekani kuendelea kuiunga mkono Serikali mpya kama ilivyofanya
kwake
·
Aishukuru
kwa misaada iliyobadilisha maisha ya Watanzania katika miaka 10 ya uongozi wake
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameihakikishia Serikali ya Marekani kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili
hautabadilika na kuwa utaendelea kuboreshwa zaidi hata baada ya kuingia madarakani
kwa Serikali mpya Novemba mwaka huu, 2015.
Aidha,
Rais Kikwete ameiomba Serikali ya Marekani kuunga mkono utawala mpya wa
Tanzania unaoingia madarakani Novemba mwaka huu kwa kiwango kile kile ambacho
Serikali hiyo imeipatia Serikali yake kwa miaka 10 iliyopita.
Vile
vile, Rais Kikwete ameishukuru Serikali na wananchi wa Marekani kwa misaada
mingi ambayo imechangia sana kuboreka kwa maisha ya Watanzania na kuinua
kiwango cha maendeleo nchini katika miaka 10 ya uongozi wake wa Tanzania.
Rais
Kikwete ameyasema hayo , Jumanne, Septemba 22, 2015 wakati alipokutana na
kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Mheshimiwa
Anthony Blinken kwenye Hoteli ya Ritz-Carlton mjini Washington ambako Rais
Kikwete amefikia katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili kwenye mji huo mkuu
wa Marekani.
Rais
Kikwete amemwambia Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani: “Sioni uwezekano
wowote wa msimamo wa Serikali mpya ya Tanzania kuhusu uhusiano wake na Marekani
kuwa tofauti na ule ambao umekuwepo katika miaka 10 iliyopita. Dhahiri uhusiano
huo hautabadilika kama Rais mpya atatoka katika chama chetu, lakini hata Rais
akitokea chama kingine, sioni kama yanaweze kuwepo mabadiliko yoyote ya msingi
ya sera au uhusiano kati ya Tanzania na Marekani.”
Kuhusu
ombi lake ya Serikali ya Marekani kuendelea kuunga mkono Serikali ijayo ya
Tanzania, Rais Kikwete amesema: “Naiomba Serikali ya Marekani iendelee
kuunga mkono Serikali yetu ijayo na wananchi wa Tanzania.”
Ameongeza:
“
Nawaombeni muendelee kuunga mkono maendeleo ya Tanzania. Matunda ya misaada
yenu sasa yameanza kuonekana. Kwa mfano katika miaka 10 iliyopita Pato la Taifa
limepanda mara tatu kutoka dola za Marekani bilioni 14.4 hadi kufikia dola za
Marekani bilioni 50 kwa sasa.”
Kuhusu
misaada ambayo Serikali ya Marekani imeitoa kwa Tanzania katika miaka 10 ya
uongozi unaomaliza muda wake, Rais Kikwete amesema: “Naishukuru sana Serikali na
wananchi wa Marekani kwa misaada mingi na kila aina ambayo mmeitoa kwa nchi
yetu na Serikali yangu. Mmeacha nyanyo
katika maendeleo ya nchi yetu. Tumepata ustawi usiokuwa wa kawaida katika miaka
10 iliyopita.”
Rais
Kikwete amesema kuwa Marekani kupitia mpango wake wa Pepfar, imechangia
kupunguza sana makali ya magonjwa ya malaria na ukimwi. “Kwa upande wa malaria, mmesaidia
kuokoa mamilioni ya maisha ya watu na vifo kutokana na ugonjwa huo sasa
vimepungua kwa kiwango cha asilimia 70. Maambukizo ya ugonjwa wa ukimwi
yamepungua sana.
Matokeo yake ni kwamba wastani wa Watanzania kuishi umepanda
kutoka miaka 55 hadi kufikia miaka 62 katika kipindi kifupi sana cha miaka 10
tu.”
Baada
ya hapo, Rais Kikwete ameingia katika undani wa misaada ya Marekani katika
maeneo mbali mbali kuanzia kwenye kilimo na mipango inayoungwa mkono na
Marekani ya Feed The Future na Alliance for Food and Nutrition Sufficiency.
“Kutokana
na misaada yenu, sasa tunajitegemea kwa chakula na hata kubakiza kiasi cha kuwauzia
majirani zetu. Na hii yote ni kwa kutilia maanani kuwa wakati tunaingia
madarakani tulilazimika kuwalisha kiasi cha watu 3.7 milioni kwa sababu ya
ukame na ukosefu wa chakula.”
Kwa
upande wa misaada iliyotolewa chini ya Mpango wa Millenium Challenge Corporation (MCC - 1), Rais amesema kuwa
misaada hiyo katika ujenzi wa barabara, usambazaji umeme na kuanzishwa kwa
miradi ya kusambaza maji imechangia mno kuboresha kiwango cha maisha ya
Watanzania.
“Chini
ya MCC, tumejenga kwa kiwango cha lami barabara zote za Pemba, tumejenga
barabara kubwa kama ile ya Tanga-Horohoro, Tunduma-Sumbawanga, Songea-Namtumbo,
tumepanua huduma za maji katika miji ya Dar es Salaam na Morogoro na
tumesambaza umeme katika mamia ya vijiji katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Mwaka 2015, ni asilimia 10 ya vijiji vyetu vilikuwa na umeme. Sasa kwa msaada
wetu, kiwango hicho kimefikia asilimia 46.”
Katika
sekta ya elimu, Marekani imesaidia upatikanaji wa vitabu vya kufundishia masomo
ya hisabati na sayansi katika shule za sekondari nchini. “Msaada wetu katika eneo hili,
umeanza kuboresha elimu yetu. Ubora wa elimu umepanda na viwango vinapanda.”
Rais
Kikwete pia ameishukuru Serikali ya Marekani kwa misaada yake katika mapambano
dhidi ya madawa ya kulevya na katika masuala ya usalama na vita dhidi ya ugaidi
akisisitiza: “kwa sababu ya misaada yenu katika eneo hili, tuko imara zaidi hata
kama matishio bado yapo.”
Rais pia ameishukuru Serikali ya
Tanzania katika ujenzi wa utawala bora yakiwemo mapambano dhidi ya rushwa. “Demokrasia
yetu inaendelea kuwa bora zaidi. Tunaendelea kupambana na rushwa, hata kama
mapambano yenyewe ni magumu. Kama mnavyojua, hata mawaziri wenzangu wawili sasa
wako jela baada ya kupatikana na hatia za matumizi mabaya ya madaraka.”
Rais
Kikwete pia ameishukuru Serikali ya Marekani kwa mchakato wa kuanzishwa kwa
Mpango wa MCC -2, akisisitiza kuwa changamoto ambazo zimejitokeza katika
maandalizi ya mpango huo zitashughulikiwa ipasavyo na kwa haraka na Serikali
yake.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24
Septemba, 2015
Umekua msemaji wetu UKAWA au????tutaamua wenyewe tushirikiane na nani na nani tupige chini!!
ReplyDelete