Ferrao.
NA MWANDISHI WETU
WADHAMINI wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, wamezitakia kila la heri timu
zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Jumamosi hii kwenye
viwanja mbalimbali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Vodacom Tanzania,Ian Ferrao, alisema kuwa ni fahari kubwa kwao
kuona msimu mpya wa ligi hiyo unaanza hivyo kutoa fursa kwa wapenzi wa soka
nchini na kwingineko kupata burudani.
Alizitaka timu zote pamoja na mchezaji mmoja
mmoja, kucheza kwa kufuata sheria zote 17 za soka ili kuutendea haki mchezo
huo, lakini pia mashabiki ambao wamekuwa wakimiminika kwa wingi viwanjani
kuzishabikia timu zao.
Ferrao aliwaonya viongozi, wachezaji na hata
waamuzi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri matokeo ya mchezo
husika, zaidi ikiwa ni rushwa na ushirikina ambao mara nyingi umekuwa
ukihusishwa katika kupunguza uhondo wa soka kwa wachezaji kutojituma uwanjani
wakiamini ‘ushindi ni lazima’.
“Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inapoanza
mwishoni mwa wiki hii, wachezaji wa timu zote shiriki, ni vema wakatambua kuwa
Vodacom inawajali ndio maana tumeongeza udhamini kutoka Sh bilioni 1.8 hadi
bilioni 2.3 ili kuifanya ligi kuwa na
msisimko wa aina yake, lakini pia kuboresha maisha ya wachezaji,” alisema.
Juu ya udhamini wao wa miaka mitatu katika ligi
hiyo, Ferrao alisema kuwa wameongeza dau kwa kuwa timu zimeongezeka kutoka 14
msimu uliopita hadi 16 msimu huu, lakini pia wakifanya hivyo ili kuiboresha na
kuongeza ushindani miongoni mwa wachezaji na timu kwa ujumla.
Ferrao aliwataka mashabiki wa soka nchini
kujitokeza kwa wingi viwanjani kuzishangilia timu zao ili kuwapandisha mzuka
wachezaji waweze kujituma kadri ya uwezo wao na kupata ushindi.
Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa watetezi
Yanga, Azam na Simba za Dar es Salaam, Mbeya City na Prisons (Mbeya), Toto
Africans (Mwanza), Kagera Sugar (Kagera), Mwadui na Stand United (Shinyanga),
Coastal Union, African Sports na Mgambo Shooting (Tanga), Mtibwa Sugar
(Morogoro), JKT Ruvu (Pwani), Ndanda FC (Mtwara) na Majimaji (Ruvuma).
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, kesho Simba
itavaana na African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Azam
watawakaribisha Prisons (Azam Complex), JKT Ruvu na Majimaji (Majimaji, Songea)
na Mgambo watakuwa wageni wa Ndanda (Nangwanda Sijaona).
Mbeya City watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar
(Sokoine), Mwadui wataifuata Toto African (Kirumba), Stand Utd wataikaribisha
Mtibwa (Kambarage), wakati mechi nyingine itachezwa Jumapili kwa Yanga
kuikaribisha Coastal Union (Uwanja wa Taifa).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...