Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi. Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. 

Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. 
Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya. Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha.

MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa. Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.

MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea. Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani. Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura.  Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote.
Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi. 
Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi.  Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu wengine. Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.

January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
28.10.2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Kipindi cha uchaguzi kinakaribia kuisha katika sehemu kubwa ya nchi, kama nchi iliyofanya uchaguzi mara nyingi, tuendelee kukomaa kisiasa na kupiga hatua mbele ya demokrasia.

    Jamani Jamani vijana kwa wazee tuelewe vurugu na uchaguzi haviendi pamoja wala tusikubali kutumiwa na yoyote kuvuriga amani au kuchoma majengo (kwanini uchome jengo? ujinga ulioje!).

    kama kuna mgombea ambaye hakuridhika aende mahakamani ni haki yake. Wanaohusika na kuboresha mapungufu yoyote yaliyojitokeza warekebishe mambo ili chaguzi zijazo ziwe za kiwango cha juu zaidi.

    Sisi wananchi tuachwe tuendelee na shughuli zetu za kila siku bila bugudha.

    Ee Mungu ibariki Tanzania.

    ReplyDelete
  2. Maana ya uchaguzi ni kupiga kura kumpata mshindi mmoja kati ya wagombea wengi wa nafasi mbali mbali kama vile nafasi ya uRais. Wananchi wa Tanzania tumetumia haki yetu kumpata Rais wetu atakaetangazwa na NEC kuiongoza nchi yetu kwa miaka mitano ijayo. Upande utakaoshindwa uonyeshe ukomavu wa kisiasa kwa kukubali matokeo na kujipanga upya kwa chaguzi zijazo baada ya miaka mitano. Wananchi wa kawaida tunahitaji amani na utilivu ili tuendelee na shughuli zetu za uzalishaji na kujikimu mahitaji yetu. Hatuhitaji malumbano yasiyo na msingi wo wote kwani hakuna aliyezaliwa na kibandiko cha uRais, uBunge n.k. Mungu ibariki Tanzania

    ReplyDelete
  3. siku zote asiyekubali kushindwa siyo mshindani. kama kweli umeshindwa ukakubali kushindwa basi hapo ndipo tunapoiona HEKIMA kama ya mfalme Suleiman inavyotumika.

    ReplyDelete
  4. Jumuiya ya Kimataifa na Waangalizi wa Kimataifa walioiwakilisha Dunia nzima wamethibitisha ya kuwa Uchaguzi Tanzania 2015 ulikuwa wa Haki,Uwazi Ukweli na Halali bila Dosari, licha ya mapungufu machache ya kawaida.

    Jumuia ya Kimataifa na Waangalizi wa Kimataifa wana Uzoefu mkubwa kufuatilia Chaguzi nyingi duniani, hawajakuja Tanzania kutekeleza jukumu lao kwa mara ya kwanza wanafahamu mambo mengi sana kuhusu Chaguzi nyingi za Dunia walizo shiriki zaidi ya sisi tunao dai Uchaguzi umeibiwa.

    Kwanza wanashangaa kwa nini Z'bar wabatilishe Uchaguzi?

    Ukishindana ktk kila jambo usitegemee kuwa lazima ushinde, kwa kawaida Mshindi anakuwa ni mmoja tu ladba kwenye Ndondi nako mnaweza kuwa droo lakini mmoja akamzidi mwenzake kwa Pointi!!!

    Wala Uchaguzi huu Tanzania 2015 kamwe hakuna Bao la mkono kama wanavyo fikiri wengi.

    TUSIPOTEZE MUDA ZAIDI ILI SHUGHULI ZA KIUCHUMI ZIREJEE KAMA KAWAIDA BAADA YA KUDORORA KUFUATIA UCHAGUZI MKUU.

    ALIYESHINDWA AENDE AKACHUNGE NGO'MBE NA KUVUA SAMAKI ANA ALIYESHINDA AINGIA IKULU TULIJENGE TAIFA LA TANZANIA.

    ReplyDelete
  5. Jumuiya ya Kimataifa na Waangalizi wa Kimataifa hawana Ubia na nchi yeyote wala Chama chochote cha Siasa Duniani.

    Kwanza jamaa ni wanoko balaa kungekuwa na dosari ni lazima wangekwenda hewani kwa kuja juu na kuishitaki Tanzania huko duniani.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...