STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 2.10.2015
MGOMBEA nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM na Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi wa
Zanzibar kuwa atakapoingia madarakani katika awamu yake ya pili ya uongozi sekta
ya michezo atazidi kuiimarisha.
Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema
hayo katika Mkutano wa CCM wa Kampeni za uchaguzi huko Kiwani, Mkoa wa Kusini
Pemba uliohudhuriwa na maelfu ya wanaCCM pamoja na wananchi yakiwemo makundi ya
vijana.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema
kuwa atahakikisha sekta ya michezo inaimarika zaidi katika kila nyanja ili
Zanzibar irudi katika asili yake ambapo Zanzibar ilitambulikana ndani na nje ya
bara la Afrika katika sekta hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa tayari kwa upande
wa Serikali Idara maalum imeshaundwa kwa ajili ya kushughulikia michezo ikiwa na
lengo la kuiimarisha sekta hiyo hapa nchini.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa lengo la
Serikali ni kuhakikisha vuguvugu la michezo linaimarika sambamba na kuwapa
kipaumbele wanafunzi ili nao wawe na muda wa kushiriki michezo.
Dk. Shein alisisitiza kuwa michezo kwa
vijana na watoto wa skuli ina umuhimu mkubwa katika kuwajenga kiafya, kiakili
pamoja na kuwajenga watoto na vijana kujenga ushirikiano, upendo na umoja
miongoni mwao.
Kutokana na umuhimu huo, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kwa kuwataka wazee kutowazuia watoto wao kushiriki michezo kutokana
na umuhimu wake mkubwa katika maisha ya mwanaadamu.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa
sekta ya michezo katika kipindi cha
miaka mitano ijayo itaimarishwa kwa mujibu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka
(2015-2020) ambapo Serikali itatekeleza mambo kadhaa kwa lengo la kuiimarisha
sekta hiyo.
Katika uongozi wa Dk. Shein Serikali
imetekeleza mambo mbali mbali katika kuimarisha sekta ya michezo ikiwa ni pamoja
na kuandaliwa kwa Sera mpya ya michezo ya Zanzibar itakayoimarisha na
kuiendeleza michezo yote.
Aidha, Serikali imeanzisha mashindano ya
riadha ya Wilaya, kwa Wilaya zote kumi za Zanzibar pamoja na kutoa vifaa mbali
mbali vya michezo kwa wanariadha wa Zanzibar ili kurejesha vuguvugu la michezo
ya riadha ambapo bado utaratibu wa kutoa vifaa hivyo unaendelea.
Pamoja na hayo, Serikali imewahamasisha
wananchi waendeleze michezo ili wajenge afya zao kwa kufanya mazoezi ya viungo
kila siku sambamba na kushiriki kwenye tamasha la mazoezi ya viungo linalofanyika
tarehe 1 Januari ya kila mwaka.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...