Kiongozi wa familia hiyo, Albert Michael, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita.

Na Rashid Zahor, Geita.
FAMILIA ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli imesema Watanzania watakuwa na bahati ya kumpata kiongozi mchapakazi, mwenye msimamo na anayependa maendeleo.

Imesema iwapo Dk. Magufuli atachaguliwa kuwa rais, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii, atawaletea maendeleo makubwa kwa kuwa ni mtu mwenye msimamo, asiyeyumba na anayependa maendeleo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na kiongozi wa familia hiyo, Albert Michael, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita.

Mzee Albert hakuwepo Katoma juzi wakati msafara wa Dk. Magufuli uliposimama kwa muda nyumbani kwa babu yake, ambako alipata nafasi ya kuzuru kaburi lake na la bibi yake mzaa wa baba na kuwaombea dua.

"Watanzania wasiwe na wasiwasi, Magufuli ni mtu anayependa watu na maendeleo na ni mchapakazi,"alisema Mzee Albert, alipokuwa akijibu swali kuhusu sifa za mgombea huyo tangu alipokuwa mtoto.

Aidha, Mzee Albert alisema Dk. Magufuli si mpole, sio mkali sana, lakini ni mtu mwenye msimamo na asiyeyumba katika jambo analotaka kulifanya.
Mzee Albert, ambaye ndiye aliyeachiwa mji wa Katoma kwa sasa, liliko chimbuko la ukoo wa Dk Magufuli, akiwa miongoni mwa wadogo zake marehemu baba mzazi wa mgombea huyo, alisema familia yao ipo pamoja naye na inamuombea Mungu aweze kutimiza dhamira yake ya kuwa rais wa awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Ninachowahakikishia Watanzania ni kwamba Oktoba 25, watampata kiongozi bora, asiye na ubaguzi wa aina yoyote,"'alisema mzee huyo.
Akizungumzia majina ya mgombea huyo, alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake siku alipozaliwa, kwa kuwa siku hiyo alikuwa akipika pombe. 

Alisema jina la Magufuli lilitokana na kupenda kwake michezo.
"Siku John alipozaliwa, bibi yake alipopelekewa taarifa, alisema 'huyo mume ni mume wangu aitwe pombe'," alisema mzee huyo, ambaye alifika Geita juzi usiku akitokea Chato.

Juzi, Dk. Magufuli alitembelea kwenye makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini na kufanya ibada ndogo ya kuwaombea dua.

Dk. Magufuli alifika nyumbani kwa babu yake saa 6.30 mchana na kupokewa na baba yake mdogo, Sylvestr Magufuli, kabla ya kupelekwa kwenye makaburi hayo, ambako aliongoza ibada ndogo ya kuwaombea dua.
Akizungumza kwenye eneo hilo, baba huyo alisema makaburi hayo ni ya babu na bibi wa mgombea huyo pamoja na ndugu zake wengine, waliofariki dunia miaka mingi iliyopita.

Alisema asili ya ukoo wa Dk. Magufuli ni Katoma, ambako ndiko baba yake alikozaliwa kabla ya kuhamishia makazi yake Chato.

"Tumezoea kumuona ndugu yetu kwenye tv na kumsikiliza kwenye redio, leo tumefurahi kumuona yeye mwenyewe,"alisema na kuongeza kuwa wanamuombea dua kwa Mungu ili aweze kuchaguliwa kuwa rais.

Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema alifarijika kufika tena katika eneo hilo kwa sababu ndiko alikozaliwa na kukulia na pia ndiko ukoo wake ulikoanzia.
Kusoma zaidi bofya HAPA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...