THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Miaka 10 inatosha kwa yeyote kutumikia Urais – Rais Kikwete
·        Awataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye kwa ari na nguvu zaidi kuliko walivyomsaidia yeye.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa miaka 10 ya uongozi inatosha kabisa kwa mkuu wa nchi kufanya mambo mengi na kuwa hahitaji muda zaidi kuweza kumaliza ajenda yake.

Aidha, Rais Kikwete amewataka watumishi wa Ikulu kumsaidia Rais ajaye hata kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata walimvyosaidia yeye katika miaka yake yote 10 ya uongozi wake.

Rais Kikwete aliyasema hayo usiku wa  Ijumaa, Oktoba 16, 2015, wakati alipozungumza na watumishi wa Ikulu katika hafla ya chakula cha jioni ambako watumishi hao waliagana na Rais Kikwete ambaye wamemtumikia kwa vipindi tofauti, wengine wakiwa wamekaa naye kwa miaka yote 10 ya uongozi wake.

Akizungumza na watumishi hao, Rais Kikwete amesema kuwa anaondoka madarakani kwa furaha sana hata kama anaona huzuni kuagana na watumishi hao wa Ikulu ambao amekaa nao kwa miaka mingi, baadhi miaka 10.

“Kwa hakika, naondoka mwenye furaha sana. Ni kweli nasikitika kuwa tunaachana lakini mambo yote mazuri yana mwisho wake. Nimeifanya kazi ya urais kwa miaka 10, nyie mnajua aina ya kazi hii.

 Miaka 10 ni mingi. Ni miaka inayotosha kabisa kwa mkuu wa nchi kukamilisha ajenda yake. Sidhani kama mtu anahitaji zaidi ya miaka 10 kutekeleza ajenda yake ya msingi,” amesema na kuongeza:

“Na hata ukitaka kukaa zaidi huwezi kuyamaliza yote. Mzee Nyerere alikaa miaka 23 hakumaliza yote na yaliyobakia alimwachia Mzee Mwinyi ambaye naye alimwachia yaliyobakia Mzee Mkapa. Rais Mkapa naye alifanya mengi lakini hakumaliza yote na akaniachia mimi. Na mimi nitamwachia yaliyobakia Rais ajaye.”

Kuhusu Rais ajaye ambaye atakuwa mkazi mpya ndani ya Ikulu, Rais Kikwete amesema: “Napenda kuwaombeni msaidieni sana Rais wetu ajaye. Kwa hakika nawaombeni tumsaidie kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata mlivyonisaidia mimi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Oktoba, 2015.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kila la kheri Rais wetu.Nadhani utapata muda wa "kupumua" sasa maana umeonyesha uvumilivu wa muda mrefu/Ukomavu wa hali ya juu.Urais siyo kazi ya kumjaribisha mtu (moderator usibane comment yangu tafadhali sina nia mbaya)

    David V

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...