RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza mshituko wake
mkubwa na huzuni yake nyingi, akiomboleza kifo cha Mbunge wa Ludewa, Mkoa wa
Njombe, Mheshimiwa Deo Filikunjombe ambaye alifariki katika ajali ya helikopta
usiku wa kuamkia leo, Ijumaa, Oktoba 16, 2015 katikati ya Hifadhi ya
Wanyamapori ya Selous, Mkoa wa Morogoro.
Katika salamu zake za
rambirambi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Anna Semamba Makinda, Rais Kikwete amesema “Nimeshtushwa mno na taarifa za kifo
cha Mheshimiwa Deo Filikunjombe. Kwa hakika, ni msiba ulionihuzunisha sana.”
Rais Kikwete
amemweleza Mama Makinda: “Tumempoteza kijana hodari na mmoja wa wabunge mahiri
ambao mchango wao katika Bunge letu tukufu na katika shughuli za uongozi wa
nchi yetu na wananchi wake zilikuwa zinajionyesha dhahiri. Ni kifo ambacho
kimetuachia pengo kubwa la uongozi na kimetokea wakati bado Bunge lako tukufu,
Chama chetu cha CCM na wananchi wa Ludewa walikuwa bado wanahitaji uongozi na
mchango wake.”
Ameongeza Rais
Kikwete: “Nakutumia wewe Spika wa Bunge letu tukufu salamu zangu za rambirambi
na kupitia kwako kwa Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao. Aidha, kupitia
kwako nawatumia wananchi wa Ludewa salamu zangu nyingi za rambirambi kwa kumpoteza
Mbunge wao na aliyewatumikia vizuri na kwa moyo wote kwa kipindi chote cha
miaka 10 ya Ubunge wake.”
Aidha, nakuomba unifikishie pole zangu nyingi
kwa familia ya Mheshimiwa Filikunjombe pamoja na ndugu na marafiki wa familia
hiyo. Naelewa machungu ya familia kwa kuondokewa na mhimili wao. Wajulishe
Wabunge, wajulishe Wana-Ludewa na ijulishe familia ya Marehemu Filikunjombe
kuwa niko nao katika maomboleza ya msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni
msiba wangu. Napenda pia wajue kuwa
naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya Marehemu
Deo Filikunjombe. Amen.
Wakati huo huo, Rais
Kikwete asubuhi ya Jumamosi, Oktoba 17, 2015, ameungana na mamia ya
wananchi na waombolezaji kuuaga mwili wa Mheshimiwa Filikunjombe katika
shughuli iliyofanyika kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) Lugalo, mjini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...