Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwisho wa uhai wa Baraza la Mawaziri kwa kadri Tanzania inavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumapili, Oktoba 25, mwaka huu, 2015.

Taarifa iliyotolewa jioni ya leo, Jumatano, Oktoba 21, 2015, Ikulu, Dar es Salaam na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Yohana Sefue imesema kuwa Serikali imetoa ufafanuzi huo kuwasaidia wananchi kuelewa maelekezo na matakwa ya Katiba na Sheria kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais na mwisho wa Baraza la Mawaziri kufuatia mijadala ya karibu katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Taarifa hiyo imekariri Ibara ya 42(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema kuwa ukiacha sababu nyingine, mtu anayechaguliwa kuwa Rais atashika madaraka ya kiti cha Urais hadi Rais Mteule atakapoapishwa.

Ibara hiyo ya 42(3) inasema: ”Mtu anayechaguliwa kuwa Rais, atashika kiti cha Rais hadi – (a) siku ambako mtu anayemfuatia katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais.”

Taarifa hiyo imesema: “Hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anaendelea kuwa Rais, akiwa na madaraka na mamlaka yote na kamili yanayoambatana na nafasi hiyo, hadi Rais Mteule anakapokula kiapo cha Urais. Hivyo, ni vyema wananchi waelewe kuwa hakutatokea wakati wowote ambapo hakuna Rais na Amiri Jeshi Mkuu mwenye mamlaka kamili na aliye tayari kuyatekeleza mamlaka hayo. Lengo ni kuhakikisha kuwa haitokei wakati wowote nchi yetu ikakosa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.”

Imesisitiza taarifa hiyo: “Madaraka na mamlaka ya Rais yapo, na hayapugui kwa namna yoyote ile, hata baada ya Uchaguzi Mkuu, mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”

Kuhusu ukomo wa Baraza la Mawaziri, taarifa imefafanua kuwa kwa mujibu wa Ibara ya  57(2) ya Katiba, Waziri na NaibuWaziri ataendelea kushikilia mamlaka ya nafasi yake hadi, ukiacha sababu nyingine, Rais mteule atakapoapishwa.

Ibara hiyo 57(2) inatamka: “Kiti cha Waziri au NaibuWaziri kitakuwa wazi litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo – (f) Ukiwadia wakati wa Rais Mteule kushika madaraka ya Rais, basi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka hayo.”

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mawaziri na NaibuMawaziri wanaendelea kushikilia nafasi zao, wakiwa na madaraka na mamlaka kamili yanayoambatana na nyadhifa zao hadi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka.

Imemalizia taarifa hiyo: “ Naomba vyombo vya habari, vyenye jukumu la kuelimisha jamii, kuwaelewesha Watanzania kuhusu utaratibu huu wakubadilishana madaraka kati ya awamu moja ya uongozi wa nchi na nyingine. Madaraka na mamlaka ya Rais yapo, na hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya uchaguzi Mkuu mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

21 Oktoba, 2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Nashukuru kwa Kurugenzi kutoa maelekezo ya Ukomo wa Urais na Uwaziri hapa nchini. Mtoa maelezo asipotoe katiba kulinda makosa ya kimakusudi na kwa makusudi kwani ni bora angekaa kimya kuliko kupotosha ukweli hali uko wazi.
    1. Kuhusu Rais ni sawa kabisa nakubaliana na maelezo yake; isipokuwa sehemu ya kuwa bado ni Amiri Jeshi mkuu hadi sasa wakati majeshi yalishamuaga hivyo kwao ni kama Raia yeyote wa Tanzania si Amiri jeshi tena.

    2.Pili kifungu cha sheria alicho nukuu 57 (2) aelezee kifungu B na E kinachoelezea kuwa waziri na Naibu waziri wanakoma mara tu Bunge linapovunjwa maana sifa mojawapo ya mtu kuwa waziri ni kuwa MB wa Tanzania. Kwanini anaruka vifungu hivyo vinavyoonyeshwa kukiukwa kimakusudi? Nafikiri Tanzania ya sasa ni ya wanaoona ni bora msemaji huyu akae kimya kuliko kuongeza hasira za watu bila sababu.Kama anamaanisha basi atoe maelekezo ya vifungu nilivyonukuu kama vinahalalisha mawaziri kuendelea na kazi zao hadi sasa!

    Keep going Michuzi Blog...

    Michael Mwasumbwe




    ReplyDelete
  2. Huu ni utaratibu wa kawaida nchi nyiingine hata baada ya kutangazwa mshindi kuna kuwa na wiki tatu za kukabidhiana madaraka na kumwezesha kiongozi mpya kuunda baraza la mawaziri na timu yake kuanza kazi. Hakuna vacuum inayoruhusiwa wakati wanaokuja wanapojipanga.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...