TANZANIA
imetimiza ndoto za kutinga hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye
makundi ya kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia, licha ya kufungwa 1-0
na Malawi jioni ya leo katika Uwanja wa Kamuzu mjini Blantyre.
Tanzania
inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya Jumatano kushinda 2-0
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya
mchujo.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de Carlvalho aliyesaidiwa
na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro Ntyamba wa Angola, hadi mapumziko
Malawi walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lilifungwa na John Banda dakika ya 42
aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Chiukepo Msowoya.
Taifa
Stars ndio walioanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya kwanza tu, mshambuliaji
Mbwana Samatta alikaribia kufunga, baada ya kumtoka beki Limbikani Mnzava,
lakini kipa Simplex Nthala akaokoa.
Malawi
wakajibu shambulizi dakika ya pili baada ya shuti kali la Banda kupanguliwa na
kipa Ally Mustafa ‘Barthez’. Barthez akafanya kazi nzuri tena dakika ya 10
baada ya kuokoa michomo miwili mfululizo ya Malawi.
Stars
ilizinduka dakika ya 35 baada ya Thomas Ulimwengu kumtoka vizuri beki wa Malawi
Yamikani Fodya baada ya pasi ndefu ya Samatta, lakini shuti lake likaenda nje
sentimita chache.
Kipindi
cha pili, kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa alianza na mabadiliko,
akimtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza mshambuliaji John Bocco.
Mabadiliko
hayo yaliifanya Stars ianze kudumu kwenye eneo la Malawi, lakini bado
mashambulizi ya hatari yalielekezwa langoni mwa Tanzania.
Dakika ya
58 Nahodha wa Tanzania, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliokoa hatari langoni mwake
na dakika ya 62 Malawi walifanya mashambulizi matatu mfululizo ya hatari lanoni
mwa Stars, ikiwemo kupata kona mbili.
Dakika ya
72 Mbwana Samatta alipiga shuti hafifu akiwa karibu na lango baada ya kupokea
pasi nzuri ya John Bocco likaenda nje.
Malawi
walifanya shambulizi la hatari dakika ya 90, lakini Robin Ngalande akashindwa
kumalizia vizuri baada ya kupiga nje.
Kwa
matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za
mchujo mwezi Novemba.
Kikosi cha
Tanzania; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Said Ndemla/John Bocco
dk46, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Mrisho Ngassa dk75.
Malawi;
Simplex Nthala, Stanley Sanudi, Miracle Gabeya/Robin Ngalande dk76, Yamkani
Fadya, Limbikani Mzava, Gerald Phiri, Chimango Kayira, Micium Mhone, Chiukepo
Msowoya, John Banda na Shumaker Kuwali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...