Na Ally Daud-Maelezo
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa vijana kutojihusisha na vitendo vya fujo katika
kipindi hiki cha kampeni badala yake waelekeze nguvu na juhudi
zaidi katika kujenga uchumi wa taifa.
Akiongea katika mkutano
uliowakutanisha NEC na wawakilishi wa vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini Makamu
Mwenyekiti wa Tume, Jaji mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Hamid Mahmoud Hamid (pichani) alisema kuwa vijana wasitumike na vyama vya siasa kama kichocheo
cha fujo .
“Vijana kamwe msikubali
kutumika kwa maslahi ya chama cha siasa ila tumieni vizuri elimu yenu na upeo
wenu wa kufikiri namna ya kujenga na kuendeleza taifa”,alisema Jaji Hamid.
Aidha Jaji Hamid aliongeza
kuwa vijana wanapaswa kuhamasisha watu mbalimbali umuhimu wa kupiga kura kwani
wao ni sehemu muhimu na ndiyo nguvu pekee inayotegemewa katika jamii ya
Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhan amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuheshimu sheria na kanuni za uchaguzi kwa mwaka huu wa 2015 ili kufanya uchaguzi kuwa haki na
amani.
“ Natoa wito kwa wananchi wa Tanzania kuepuka kuingilia kazi za watumishi wa Tume ya uchaguzi
kwa kuhakikisha kuwa kila mwananchi atapiga kura katika kituo alichojiandikisha
ili kuepusha usumbufu “ alisema Bw. Ramadhan .
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi imeweka utaratibu maalum wa namna ya kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Octoba 25 mwaka
huu kwa ngazi ya Rais, Wabunge na
Madiwani ambapo madiwani watatangazwa na mkurugenzi wa NEC ngazi ya kata,
Wabunge ngazi ya Jimbo na Rais atatangazwa na Tume ya Uchaguzi (NEC).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...