Marehemu Deo Filikunjombe.


SAFARI ya aliyekuwa mbunge mahiri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe, hapa duniani, ilikamilika jana saa 10.30 jioni wakati mwili wake ulipozikwa kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki mjini Ludewa, katika jimbo ambalo aliliongoza kwa ufanisi mkubwa kwa miaka mitano iliyopita.
Vilio, huzuni, simanzi vilitawala wakati wa maziko ya mwanasiasa huyo kijana ambaye alizikwa pamoja na wenzake wawili wanaotajwa kwamba walikuwa watu wake wa karibu. 
Filikunjombe (43) aliyeiongoza Ludewa kuanzia mwaka 2010 hadi Agosti mwaka huu, na aliyekuwa akitetea kiti chake katika Uchaguzi Mkuu wa Jumapili wiki hii, alikufa katika ajali ya helikopta iliyotokea Alhamisi wiki iliyopita baada ya kuanguka kwenye Pori la Akiba la Selous mkoani Morogoro akitokea Dar es Saaam kwenda Ludewa.
Spika Anne Makinda aliongoza mamia ya wananchi wa Ludewa waliojitokeza kumzika mpendwa wao huyo, pamoja na wenzake wawili, Egid Nkwera (43) na Cansablanca Haule (53), waliokufa pamoja katika ajali ya helikopta yenye usajili wa namba 5Y-DDK ambayo pia ilichukua uhai wa rubani wake, Kapteni William Silaa ambaye ni baba wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Jerry Silaa.
Jerry pia ni mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam na alikuwa Meya wa Manispaa ya Ilala katika uongozi uliomalizika hivi karibuni. Baba yake alitarajiwa kuzikwa jana jijini.
Filikunjombe na wenzake walizikwa saa 10.30 jioni katika makaburi ya Kanisa Katoliki, ambako Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe, Alfred Maluma, aliendesha misa ya maziko, huku akiwataka wana Ludewa na familia kujipa moyo na kumwomba Mungu awasaidie katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao.
Akimzungumzia Filikunjombe, Spika Makinda alisema alikuwa ni nyota ambayo ilianza kung’ara, alikuwa kijana mdogo aliyekuwa anawapenda wananchi wake wa Ludewa na Taifa kwa ujumla katika utumishi wake wa uwakilishi bungeni.
Makinda alisema anatamani kama Filikunjombe angeongoza wananchi wake kwa miaka 20 zaidi kama yeye alivyoongoza Jimbo la Njombe Kusini ili kukamilisha mipango yake kuwaletea maendeleo wa wananchi.
Viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria maziko hayo ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Akitoa salamu zake, Zitto alisema wananchi wa Ludewa ni vigumu kumpata kiongozi wa aina ya Filikunjombe ambaye alikuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao.
Filikunjombe na Zitto walijipatia umaarufu wakati wa sakata la Escrow mwishoni mwa mwaka jana, Zitto akiwa Mwenyekiti wa PAC huku Filikunjombe akiwa Makamu wake, kutokana na msimamo wao wa kutaka wahusika wote wa kashfa hiyo iliyohusisha uchotwaji wa Sh bilioni 306, wachukuliwe hatua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...