Kwa mujibu wa  Sheria ya Sikukuu za Kitaifa  (The Public Holidays Act, Cap 35) pamoja na Sheria zingine zinazompa mamlaka Rais kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri zitakazofanyika tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike  kwa kufanya kazi.  

Kwamba maadhimisho ya Uhuru ya mwaka huu  (2015) yatatumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi (Uhuru na Kazi) katika Taifa letu.  Mheshimiwa Rais ameelekeza Watanzania wote siku hiyo waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.

Aidha, kwa kuwa Sherehe za Uhuru na Jamhuri huendana na Maandalizi mbalimbali ambayo yanatumia fedha, kwa kuzingatia kuwa siku hiyo itaadhimishwa kwa kufanya kazi,  fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali n.k. kadri kamati za maandalizi zitakavyoamua.

Ieleweke kuwa sherehe za Uhuru na Jamhuri ni muhimu katika kuadhimisha kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu. Hivyo,   sherehe hizi zitaendelea kuadhimishwa kila mwaka kama kawaida kuanzia mwaka 2016.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kusheherekea uhuru kuendane na sura ya uhuru. Kipindupindu kama ni adui maradhi hongera rais. Bila shaka walioleta dhana ya ukombozi wa pili wa watanzania hawatapinga. Hongera Magufuli.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...