Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akitoa taarifa kwa wananchi baada ya Chadema Kufungua Kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga kuzuiliwa kwa mwili wa Marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza.

Na George Binagi - GB Pazzo wa Binagi Media Group

Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema leo kimefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, ili kuiomba Mahakama hiyo kutengua zuio la kuuaga mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita Marehemu Alphonce Mawazo, lililotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kutokana na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa ugonjwa wa Kipindupindu.

Katika kesi hiyo, Chadema inawakilishwa na Mawakili watatu ambao ni James Millya, John Mallya pamoja na Paul Kipeja ambapo mlalamikaji ni Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo.

Mahamaka hiyo chini ya Jaji Lameck Mlacha, imesikiliza malalamiko ya upande wa washtaki na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo imeamuru mlalamikiwa ambae ni Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mwanza pamoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali kupelekewa nyaraka za kesi hiyo kabla ya kusikiliza utetezi wao hapo kesho.

Mapema kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamekusanyika nje ya viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, walilalamikia hatua ya jeshi la polisi kuwazuia kuingia Mahakamani hapo ili kujua hatima ya kesi hiyo, ambapo wamesema kitendo hicho kinaondoa dhana ya Rais John Pombe Magufuli, kuwa yeye ni rais wa wananchi wote wakati wao kama Chadema wananyimwa haki zao.

Licha ya Malalamiko hayo pamoja na ulinzi mkali wa polisi uliokuwa umetanda Mahakamani hapo, bado wafuasi wa Chadema hawakuondoka katika viunga vya Mahakama hiyo hadi pale Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Freeman Mbowe alipowasihi kurejea majumbani mwao hadi kesho kesi hiyo itakaposikilizwa tena.

Ni zaidi ya siku nane sasa tangu marehemu Alphonce Mawazo auawe kikatili Mkoani Geita na watu wasiojulikana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni chuki za kisiasa ambapo mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Mmoja wa Mawakili wa Chadema John Mallya akitoa taarifa ya kesi baada ya Chadema Kufungua Kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kupinga kuzuiliwa kwa mwili wa Marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Huu ni uonevu wa waziwazi.

    Nina hakika Raisi Magufuli haungi mkono vitendo hivi viovu vya jeshi la polisi.

    Hata katika hotuba yake bungeni Raisi Magufuli aliviasa vyombo vya dola, haswa polisi, viache kunyanyasa wananchi.

    Chadema waachwe wakamzike kiongozi na wasisumbuliwe.

    ReplyDelete
  2. Yaani hata Mawakili huko Mwanza wanatokea huko huko mkoani Chadema?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...