Na George Binagi - GB Pazzo wa Binagi Media Group
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo Chadema leo kimefungua kesi katika Mahakama
Kuu Kanda ya Mwanza, ili kuiomba Mahakama hiyo kutengua zuio la kuuaga
mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita Marehemu
Alphonce Mawazo, lililotolewa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kutokana
na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa ugonjwa wa Kipindupindu.
Katika
kesi hiyo, Chadema inawakilishwa na Mawakili watatu ambao ni James
Millya, John Mallya pamoja na Paul Kipeja ambapo mlalamikaji ni Charles
Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo.
Mahamaka
hiyo chini ya Jaji Lameck Mlacha, imesikiliza malalamiko ya upande wa
washtaki na kuahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo imeamuru mlalamikiwa
ambae ni Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mwanza pamoja na mwanasheria Mkuu wa
Serikali kupelekewa nyaraka za kesi hiyo kabla ya kusikiliza utetezi wao
hapo kesho.
Mapema kabla ya kesi hiyo kusikilizwa,
wafuasi wa Chadema waliokuwa wamekusanyika nje ya viunga vya Mahakama
Kuu Kanda ya Mwanza, walilalamikia hatua ya jeshi la polisi kuwazuia
kuingia Mahakamani hapo ili kujua hatima ya kesi hiyo, ambapo wamesema
kitendo hicho kinaondoa dhana ya Rais John Pombe Magufuli, kuwa yeye ni
rais wa wananchi wote wakati wao kama Chadema wananyimwa haki zao.
Licha
ya Malalamiko hayo pamoja na ulinzi mkali wa polisi uliokuwa umetanda
Mahakamani hapo, bado wafuasi wa Chadema hawakuondoka katika viunga vya
Mahakama hiyo hadi pale Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Freeman Mbowe
alipowasihi kurejea majumbani mwao hadi kesho kesi hiyo itakaposikilizwa
tena.
Ni zaidi ya siku nane sasa tangu marehemu Alphonce
Mawazo auawe kikatili Mkoani Geita na watu wasiojulikana kutokana na
kile kilichoelezwa kuwa ni chuki za kisiasa ambapo mwili wake
umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Huu ni uonevu wa waziwazi.
ReplyDeleteNina hakika Raisi Magufuli haungi mkono vitendo hivi viovu vya jeshi la polisi.
Hata katika hotuba yake bungeni Raisi Magufuli aliviasa vyombo vya dola, haswa polisi, viache kunyanyasa wananchi.
Chadema waachwe wakamzike kiongozi na wasisumbuliwe.
Yaani hata Mawakili huko Mwanza wanatokea huko huko mkoani Chadema?
ReplyDelete