JESHI la Polisi kanda maalum ya Dar es salaam imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 7 wakiwa na silaha 8 na risasi 62 kwenye msako uliofanyika jijini Dar es salaam katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akiongea na waandishi wa habari leo, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kamishna wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova amesema wahalifu walidhani kuwa Jeshi la Polisi limeweka nguvu katika uchaguzi mkuu na kusahau kufanya misako yake iliyokuwa ikifanya mara kwa mara kama moja ya majukumu yake.
“Ukweli ni kwamba Jeshi la Polisi lilijipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na misako mingine inaendelea kufanyika kama kawaida kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na mikoa ya jirani” Alisema kamanda Kova.
Kamanda Kova aliongezea kwa kusema kuwa, Jeshi la Polisi kanda maalum inashirikiana na mikoa ya jirani kuhakikisha kuwa watuhumiwa hao hawapati fursa ya kukwepa mkondo wa sheria.
Aidha alizitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni SMG moja (1), Bastola sita (6) na Mark 4 riffle moja (1) na risasi 62 ambapo mpaka sasa jumla ya majambazi 74 wamekamatwa ikiwa ni pamoja na silaha 51 na risasi 890 za silaha mbalimbali.
Kamanda Kova amezidi kufafanua kuwa kutakuwa na msako mwingine mkali kuelekea sikukuu za x-mass na mwaka mpya 2016, utakayofanyika katika mikoa ya kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke wakisaidiwa na vikosi maalum vilivyopo Kanda ya Dar es Salaam.
Msako huo utajikita katika kuwakamata majambazi, magaidi, wanaojihusisha na madawa ya kulevya, vibaka, wapiga debe, wanaouza pombe haramu, madanguru yote ambayo pia huhifadhi wahalifu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...